Netanyahu, Gantz wakaribia kuunda serikali ya umoja
27 Machi 2020Hatua ya Gantz inaonekana kuashiria kumpa nafasi Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu ya kuendelea kusalia mamlakani na kuendeleza utawala wake wa miaka 11, japo hakuna makubaliano yoyote yaliyotangazwa kuhusu hilo.
Vile vile hatua hiyo imesababisha mpasuko wa kisiasa katika kambi inayompinga Netanyahu ambaye ameshtakiwa kwa tuhuma za ufisadi.
Kufuatia hatua hiyo, Mshirika wa Gantz, Yair Lapid ameamua kuvunja uhusiano wake wa kisiasa na mkuu huyo wa zamani wa jeshi na kumshtumu kwa kusalimu amri bila ya mapambano.
Lapid pia ametangaza wazi kuvunjika kwa muungano wa Bluu na Nyeupe ambao ulikuwa unaongozwa na Gantz.
Washirika wawili katika muungano wa Bluu na Nyeupe, vyama vya Telem na Yesh Atid vilitangaza kuondoka kwenye muungano huo.
Vyanzo kutoka muungano huo vililiambia shirika la habari la AFP kuwa jina la muungano huo litasalia kuwa hilo hilo, japo hawamtambui tena Gantz kama kiongozi wao.
Gantz na Netanyahu wamekuwa katika mapambano makali ya kisiasa mwaka uliopita huku wote wawili wakishindwa kuibuka na ushindi wa moja kwa moja katika chaguzi tatu zilizopita.
Wanasiasa hao walikosa kupata uungwaji mkono ambao ungewazesha kuunda serikali ya mseto.
Gantz alikabidhiwa jukumu la kuunda serikali baada ya uchaguzi wa Machi lakini akashindwa kufanya hivyo baada ya chaguzi mbili zilizopita.
Aidha hakukuwepo uhakika wowote kuwa angefanikiwa kuunda serikali wakati huu hasa ukizingatia mpasuko uliopo katika kambi yake ya kisiasa.
Hata hivyo licha ya mgawanyiko uliopo katika kambi ya Gantz ambayo ilikuwa na wingi wa viti katika bunge la Israel ulilazimisha kutimuliwa kwa aliyekuwa spika wa bunge hilo Yuli Edelstein ambaye ni mwanachama wa Likud, chama anachokiongoza Netanyahu.
Baada ya kutimuliwa kwa Edelstein kama spika, Gantz alijitolea kuchukua nafasi yake, uamuzi ambao umetafsiriwa kuwa amekubali hawezi kuchaguliwa kuwa Waziri Mkuu.
Nyakati zisizi za kawaida
Baada ya kuchaguliwa kama spika, Gantz aliliambia bunge kuwa "hizi ni nyakati zisizo za kawaida, na zinahitaji mtu kuchukua maamuzi ambayo sio ya kawaida” mwisho wa nukuu.
Nacho chama cha Lukid kupitia taarifa hakikukataa kuwa mazungumzo kuhusu kubuniwa kwa serikali ya umoja yamefanyika lakini chama hicho kimepuzilia mbali juu ya upangaji wa serikali hiyo kwa kusema ni uvumi tu.
Mpangilio wa kubuniwa kwa serikali hiyo ya umoja huenda ukawa ni wa muda mfupi, labda katika kipindi hiki ambacho ulimwengu unatikiswa na janga la Corona.
Israel imerekodi zaidi ya visa 2,600 ya maambukizi ya virusi vya Corona huku ikiweka marufuku ya watu kutotoka nje bila sababu maalum ili kuzuia kuenea kwa virusi hivyo.
Gantz hata hivyo anaonekana kuwa na imani kuwa muungano huo utasalia kuwa imara licha ya mpasuko uliojitokeza akisema kuwa atafanya kila awezalo kuhakikisha mshikamano unapatikana.