Netanyahu aomba kinga dhidi ya kesi ya rushwa
2 Januari 2020Netanyahu anayekabiliwa na kiwingu cha mashtaka ya rushwa na mbinyo kutoka chama cha upinzani cha mrengo wa wastani amewaambia waandishi habari mjini Jerusalem kuwa kinga hiyo itamuwezesha kuendelea kuitumikia Israel.
Msemaji wake Ofer Golan amethibitisha kuwa ombi hilo tayari limewasilishwa kwa spika wa bunge la Israel, Knesset.
Netanyahu mwenyewe amesema ombi lake limezingatia sheria na linalenga kuhakikisha anaendelea kuwa na uwezo wa kuitumia nchi hiyo kwa maslahi yake za siku za usoni.
"Ninaomba kinga kwa sababu nimeyatoa sadaka maisha yangu kwenu ninyi watu wa Israel. Lakini wako watu ambao tofauti na mimi wamefanya uhalifu mkubwa na wanayo kinga ya maisha. Kwa sababu wako kwenye nafasi nzuri mbele ya vyombo vya habari na mrengo wa kushoto" amesema Netanyahu mjini Jerusalem
Mashtaka dhidi yake yatacheleweshwa
Ombi la kupatiwa kinga linatarajiwa kuchelewesha kwa miezi kadhaa kuanza kusikilizwa kwa kesi inayomkabili kwa sababu wabunge hawawezi kulipigia kura hadi baada ya uchaguzi mkuu wa mwezi Machi.
Netanyahu alishatakiwa na mwanasheria mkuu wa serikali Novemba iliyopita kwa makosa matatu tofauti yanayojumuisha rushwa, udanganyifu na kupoteza uaminifu.
Kiongozi huyo wa chama cha mrengo wa kulia cha Likud ambaye pia ni waziri mkuu aliyehuduhumu kwa muda mrefu nchini Israel amesema mara kadhaa kuwa na mashataka dhidi yake yamechochewa kisiasa.
Madai dhidi ya waziri mkuu huyo yanajumuisha kupokea zawadi zenye thamani ya maelfu ya dola pamoja na kuridhia kubadili kanuni kwa lengo la kupatiwa upendeleo kwenye maudhui ya vyombo vya habari.
Licha ya mashtaka yanayomkabili, Netanyahu amesalia kuwa mashuhuri ndani ya chama chake cha Likud na wiki iliyopita alipata ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa ndani ya chama.
Hasimu wake amkalia kooni
Akizungumzia ombi hilo, hasimu mkuu wa Netanyahu, Benny Gantz ambaye kiongozi wa chama cha mrengo wa wastani cha Buluu na nyeupe, amesema waziri mkuu huyo anafahamu kwamba ana hatia.
Gantz amesema chama anachokiongoza kitafanya lolote linalowezekana kuhakikisha Netanyahu hapatiwi kinga hiyo.
"Ninaona Israel leo inaongozwa na mtu aliye tayari kutusukuma ukingoni na kutishia msingi wa kiraia ambao sote tumefunzwa kwamba kila mtu yuko sawa mbele ya sheria". amesema Gantz kwenye mutano na waandishi habari.
Hata hivyo, wataalamu wa sheria wameiomba mahakama ya juu kutoa uamuzi iwapo waziri mkuu anaweza kupewa majukumu na rais ya kuunda serikali wakati akiwa anakabiliwa na mashtaka.
Jopo la majaji watatu limekuwa likitathmini suala hilo na limesema litatoa uamuzi kaitkia siku zinazokuja bila kutaja tarehe rasmi.