Netanyahu akubali kupeleka wajumbe wa Israel Misri na Qatar
29 Machi 2024Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amekubali kutuma ujumbe wa Israel nchini Misri na Qatar, ambako wapatanishi wamekuwa wakitafuta mbinu za kuachiwa huru watu waliochukuliwa mateka na Hamas, kama sehemu ya makubaliano yanayotafutwa ya kusitisha mapigano kwa muda ili misaada zaidi pia iweze kufikishwa Gaza.
Ofisi ya Netanyahu imesema Waziri Mkuu huyo alizungumza na wakuu wa taasisi ya usalama ya Israel Shin Bet na kiongozi wa shirika la ujasusi la Israel Mossad na kuidhinisha ujumbe wa Israel, kuondoka katika siku kadhaa zijazo kuelekea Doha na Cairo ili kuendeleza mazungumzo hayo.
Wapatanishi kutoka Marekani, Misri na Qatar wamejaribu kupata suluhu ya mgogoro unaoendelea Gaza lakini mazungumzo yaliyoanzishwa yanaonekana kukwama ikiwa ni takriban siku ishirini baada ya kuanza mwezi mtukufu wa Ramadhan uliyo muhimu kwa waumini wa kiislamu.