Netanyahu aahidi kupambana dhidi ya mashtaka ya rushwa
10 Desemba 2024Netanyahu alipanda kizimbani leo kuanza kutoa ushahidi katika kesi ya muda mrefu inayomkabili. Amekuwa kiongozi wa kwanza wa Israel aliyeko madarakani kupandishwa kizimbani akikabiliwa na kesi ya jinai.
Katika ushahidi wake wa ufunguzi kwenye mahakama iliyojaa watu mjini Tel Aviv, Netanyahu alihoji kuwa yeye ni kiongozi aliyejitolea na mtetezi wa maslahi ya Israel, akiyataja mashitaka yanayomkabili kuwa ni kama tone baharini ikilinganishwa na changamoto alizopitia wakati akiilinda nchi yake.
Netanyahu, mwenye umri wa miaka 75, anajibu mashtaka ya udanganyifu, kuvunja uaminifu na kupokea rushwa katika kesi tatu tofauti zinazomkabili.
Ameiambia mahakama kuwa atamudu kuhudhuria vikao vya kesi yake mahakamani na wakati huo huo kuendelea kutekeleza majukumu yake ya uwaziri mkuu katika wakati ambao Israel iko vitani huko Gaza.