1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Sheria na HakiUlaya

Nchi za Magharibi washutumu Urusi kufuatia kifo cha Navalny

Hawa Bihoga
17 Februari 2024

Mataifa ya Magharibi yameendelea kuweka shinikizo kwa Urusi, yakimshutumu Rais Vladmir Putin na serikali yake kuhusika na kifo chenye utata cha mkosoaji mkuu wa ikulu ya Kremlin, Alexei Navalny.

https://p.dw.com/p/4cWG5
Munich, Ujerumani | Waandamanaji wanaokosoa kifo cha Alexei Navalny
Maandamano yanayopinga kifo cha mkosoaji wa Ikulu ya Kremlin Alexei NavalnyPicha: Peter Kneffel/dpa/picture alliance

Rais wa Marekani Joe Biden kupitia ukurasa wa mtandao wa X zamani Twitter amemshutumu waziwazi rais Putin akisema ndiye "anahusika na kifo cha Navalny", huku mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, Dmitry Muratov akiongeza kuwa mkosoaji huyo wa Putin "aliteswa kwa miaka mitatu na kwamba mauaji yameongezwa kwenye kifungo cha Navalny."

Mashirika ya habari nchini Urusi yanaripoti kwamba jopo la madaktari walijaribu kuokoa maisha ya Navalvy kwa takriban nusu saa lakini ilishindikana kutokana na kile kichotajwa na maafisa wa gereza kuwa "alijihisi vibaya na kupoteza fahamu".

Soma pia:Alexei Navalny afariki akiwa gerezani

Mkewe Yulia Navalny ameitaka Jumuiya ya kimataifa kuungana na kuushinda utawala "mbaya na wa kutisha" wa Putin.

Hata hivyo Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov aliwashutumu viongozi wa nchi za Magharibi kwa "mwitikio usiokubalika" juu ya kifo cha Navalny.