1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi za Magharibi hazijaridhishwa na serikali ya Taliban

8 Septemba 2021

Ujerumani, China, Japan na Umoja wa Ulaya hawakuridhishwa na serikali ya mpito ya Taliban nchini Afganistan, kufuatia kundi hilo lenye misimamo mikali ya kidini kuchukua udhibiti wa mji mkuu wa Kabul mwezi uliopita.

https://p.dw.com/p/404vX
Afghanistan Kabul | PK der Taliban: Sprecher Zabihullah Mujahid: Mullah Mohammad Hasan Akhundzada soll Taliban leiten
Picha: AAMIR QURESHI/AFP/Getty Images

Viongozi wa Taliban pekee ndiyo walioteuliwa kushika nyadhifa za juu za serikali hiyo - ambayo haijumuishi wanawake wala mtu yoyote kutoka nje ya kundi hilo. Si hayo tu, mshirika wa karibu wa mwanzilishi wa kikundi hicho ndiye aliyeteuliwa kuwa waziri mkuu huku waziri wa mambo ya ndani akiwa kwenye orodha ya magaidi ya Marekani.

Muundo wa serikali hiyo mpya unapingana na ushauri liliopewa kundi la Taliban na mataifa yenye nguvu ulimwengu wa kuunda serikali inayojumuisha makundi tofauti ya jamii ya Afghanistan.

Akieleza wasiwasi wake kuhusu muundo wa serikali hiyo mpya, waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas amekiri kuwa tangu awali hakuwa na matumaini makubwa ya hali kubadilika Afghansitan.

Ujerumani kuendelea kuzungumza na Taliban

Maas amesema tangazo la serikali ya mpito bila ya kushirikishwa vikundi vingine, na nguvu iliyotumiwa na Taliban wiki hii dhidi ya  waandamanaji na waandishi wa habari huko mjini Kabul, ni ishara ambazo hazitoi matumaini.

Maas amesema, Ujerumani hata hivyo itaendelea kuzungumza na kundi hilo ili kuhakikisha watu wanaendelea kuruhusiwa kuondoka Afghanistan, kwani hakukaliki kutokana na uhaba wa chakula na kusimamishwa kwa misaada ya kimataifa.

Deutschland Bundestag Angela Merkel
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Mbali na Ujerumani, Umoja wa Ulaya kwa jumla umesemaserikali mpya ya mpito ya kundi la Taliban Afganistan haikuheshimu ahadi zao walizozitoa za kuunda serikali inayojumuisha makundi yote nchini humo.

Wanawake wa Afghanistan binafsi waliandamana baada ya kutangazwa baraza la mawaziri lisilokuwa na mwanamke hata mmoja.

Kwa bahati mbaya, usiku wa Jumanne, wakati baraza la mawaziri lilipotangazwa, ilibainika kuwa wanawake hawana sehemu yoyote katika baraza la mawaziri, na kwamba sio tu hakuna wanawake katika baraza la mawaziri, lakini serikali iliyotangazwa haishirikishi makundi mengine, hii ni serikali ya kundi moja tu.

Japan kuendelea kushirikiana na Marekani na nchi zengine

China ambayo inapakana na Afganistan, imewasisitizia viongozi Taliban kuunda serikali yenye uwazi na inayojumuisha makundi tofauti baada ya kundi hilo kuchukua madaraka kufuatia kuondoka kwa vikosi vya Marekani vilivyoivamia nchi hiyo kwa miaka 20.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa China Wang Wenbin amesema kwamba China inauangalia uteuzi wa serikali mpya kama hatua muhimu utakaorahisisha kuijenga tena  Afghanistan.

Wang ameongeza kuwa China iko tayari kuendelea kufanya mazungumzo na viongozi wa serikali hiyo mpya.

Nchini Japan, afisa wa ngazi ya juu amesema nchi yake imekuwa ikifuatilia hatua za kundi la Taliban na itaendelea  kushirikiana na Marekani na nchi zingine, licha ya kuwa na wasiwasi kuhusu usalama wa raia nchini Afghanistan.

Afghanistan Kabul | Demonstration gegen Pakistan
Mwanamgambo wa Taliban akiwakabili waandamanaji KabulPicha: REUTERS

Aidha Mkuu wa Baraza la Mawaziri Katsunobu Kato ameongeza kwamba, kupitia juhudi mbali mbali, pamoja na mazungumzo na Taliban, wanafanya bidii kuhakikisha usalama wa raia wa Japan na wa wafanyikazi wa Kiafghani ambao wamebakia nchini humo. Pia ameahidi kuwasaidia Wajapani wanaotaka kuondoka nchini Afghanistan.

Hali haitajwi kuwa ni nzuri katika taifa hilo la katikati mwa bara la Asia. Kwani Umoja wa Mataifa umesema huduma za msingi zimekuwa ngumu kupatikana. Chakula na misaada mengine muhimu vyote vinakaribia kuisha. Mbali na hayo, zaidi ya watu nusu milioni wameshapoteza makazi yao Afghanistan kwa mwaka huu pekee.

Vyanzo: afp,rtre,ebu