1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi za Kiafrika hazitumii nafasi ya mkataba wa AGOA

5 Agosti 2010

Mkataba wa AGOA hutoa nafasi kwa mataifa ya Kiafrika kusafirisha zaidi ya aina za bidhaa 6,400 nchini Marekani bila kulipa ushuru.

https://p.dw.com/p/OcVm
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani, Hillary Clinton.Picha: AP

Vikwazo vya kibiashara, miundo mbinu mibovu na rushwa ni kati ya mambo yanayoziregesha nyuma harakati za kuimarisha biashara katika bara la Afrika. Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Hillary Clinton aliyasema hayo katika mkutano wa kila mwaka unaozijadili hatua zilizofikiwa chini ya makubaliano ya kuimarisha biashara kati ya bara la Afrika katika soko la Marekani unaojulikana pia kama AGOA.

Bibi Clinton akiapa kulisaidia bara la Afrika kuepuka umaskini, alisema mkakati wa kibiashara na maendeleo wa utawala wa rais Barack Obama unasisitiza juu ya kupanua biashara ya kikanda barani humo, kuendeleza matumizi bora ya misaada na pia kushirikiana na serikali za Kiafrika ili kuhakikisha kuna mabadiliko na hatimaye kuwa na soko huru.

Akizungumza katika mkutano wa kila mwaka wa mkataba juu ya ukuaji wa uchumi wa bara la Afrika na nafasi za kibiashara katika soko la Marekani, unaojulikana pia kama AGOA, ambao unaziruhusu nchi zilizo katika eneo la kusini mwa jangwa la sahara kusafirisha zaidi ya aina za bidhaa 6,400 nchini Marekani bila ya kulipa ushuru, waziri huyo wa mambo ya kigeni wa Marekani alisema mkataba huo bado haujayafikia matumaini yaliyotarajiwa ya kupanua biashara.

Akizungumza na maafisa wakuu wa Kiafrika na viongozi wa kibiashara, Bibi Clinton alisema bidhaa zinazotokana na mafuta ndizo zinachangia asilimia kubwa ya bidhaa zinazosafirishwa nchini Marekani na kwamba hawajaona mataifa ya bara la Afrika yakiongeza usafirishaji wa bidhaa zingine.

Mwakilishi wa kibiashara wa Marekani, Ron Kirk alisema mkataba huo wa AGOA unaweza ukaongezewa muda na bunge la Marekani kabla ya muda unaotarajiwa kukamilika mwaka wa 2015, ingawa haiwezekani ikawa mkataba wa kudumu. Makundi ya kibiashara ya Kiafrika yanasema kwamba asili ya mkataba huo ambayo sio ya kudumu, inakatiza motisha ya uwekezaji wa muda mrefu katika bara hilo.

Bibi Clinton alisema uchumi wa mataifa ya kusini mwa jangwa la Sahara unaweza kukua haraka zaidi ya mataifa ya kusini mwa Marekani, Uropa au Marekani mwaka huu. Hata hivyo alilalamika kwamba bara la Afrika kama kanda ambayo ina asilimia 12 ya idadi ya watu duniani, inatoa chini ya asilimia mbili tu ya pato jumla duniani.

Waziri Clinton ambaye alizizuru Angola, Kenya, Liberia, Nigeria na mataifa mengine ya Kiafrika mwaka jana, alisema Afrika inafaa kuboresha barabara, kuimarisha usafiri wa ndege uwe wa haraka na pia kuongeza viwango vya nishati ili viweze kusaidia biashara. Alisema kwamba rushwa huigharimu bara hilo kima cha Dola milioni 150 kila mwaka na mara nyingi huwatoa ari wawekezaji, inavuruga ubunifu na inapunguza kasi ya ukuaji wa biashara.

Waziri huyo alitoa mfano wa Jumuiya ya Afrika mashariki kama ishara nzuri ya kupanua biashara Kikanda. Jumuiya hiyo inayozihusisha Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi ina soko la watu milioni 127 na pato jumla la Dola bilioni 73. Kiwango cha biashara katika Jumuiya hiyo kimeongezeka kwa asilimia 50 tangu kuundwa kwa soko la pamoja mwaka wa 2005, kupunguzwa ushuru na kuoanisha sera za kibiashara.

Mwandishi, Peter Moss /Reuters

Mhariri, Mwadzaya,Thelma