1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi za ACP zina wasi wasi na Makubaliano ya Doha

P.Martin21 Mei 2008

Kuna matumaini ya kupatikana makubaliano ya kimataifa ya biashara yanayongojewa na WTO -Shirika la Biashara Duniani- tangu majadiliano kuanzishwa hapo mwaka 2001 katika mji mkuu wa Qatar Doha.

https://p.dw.com/p/E3Wk
Mkurugenzi mkuu wa shirika la biashara dunaini WTO,Pascal Lamy (kulia)Picha: AP

Ukweli ni kwamba baadhi ya nchi zinazoendelea katika kanda ya Afrika,Karibik na Pacifik kwa ufupi ACP, zina wasi wasi kuwa makubaliano ya kufungua zaidi masoko yao kwa bidhaa za nchi tajiri huenda kukasababisha matatizo makubwa hasa wakati huu ambapo nchi masikini zinapambana na mzozo wa chakula.

Kwani azma ya Duru ya majadiliano ya Doha ya WTO iliyoanza mwaka 2001 ni kupunguza vizingiti vya biashara-yaani nchi zinazoendelea zipunguze ushuru wa forodha kwa bidhaa za viwandani kutoka nchi tajiri.Na bidhaa za nchi zinazoendelea zitaruhusiwa kuingia katika masoko ya nchi tajiri kwa urahisi zaidi.

Majadiliano hayo yalitazamiwa kukamilishwa na mkataba kutiwa saini hapo mwaka 2004.Lakini mazungumzo hayo yamekwama hadi hivi sasa kwa sababu nchi tajiri na zile zinazoendelea zimeshindwa kukubaliana kuhusu ushuru wa forodha utakaotozwa kwa mazao ya viwandani kutoka nchi tajiri.Vile vile baadhi ya nchi za ACP zinalalamika kuhusu ruzuku inayolipwa kwa wakulima katika nchi tajiri.Nchi zinazoendelea zinasema,mazao yao ya kilimo hayawezi kushindana na mazao ya wakulima wa nchi tajiri wanaosaidiwa kifedha na serikali zao.Si hilo,kwani serikali za ACP zitapungukiwa na pato lake iwapo zitashusha ushuru wa forodha kwa kiwango kinachodaiwa.

Hata uchunguzi uliofanywa na Benki Kuu ya Dunia mwaka 2005 na vile vile Umoja wa Ulaya katika mwaka 2006, umeonyesha kuwa nchi za ACP zitapata hasara hata ikiwa bidhaa zao zitaruhusiwa kuingia kwa urahisi zaidi katika masoko ya nchi za Ulaya.

Sasa ndio WTO imefanya marekebisho - na mapendekezo mapya yamewasilishwa mkutanoni mjini Geneva katika jitahada ya kuweka msingi wa maafikiano.Ni matumaini ya WTO kuwa mkataba wa biashara utaweza kutiwa saini na nchi wanachama 152 wa shirika hilo la biashara duniani ifikapo mwisho wa mwaka huu.