G7 latumia mabilioni kuendeleza sekta ya nishati asilia
4 Juni 2018Ripoti hiyo imetolewa Jumatatu kuelekea mkutano wa kilele wa mataifa yaliyoendelea kiviwanda duniani wa kundi la G7 utakaofanyika nchini Canada, Juni 8-9.
Uingereza, Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japan na Marekani - mataifa yanayojulikana kama kundi la G7- yalitoa ahadi mnamo mwkaa 2016 kusitisha kuunga mkono utumiaji wa nishati za asili ifikapo mwaka 2025.
Lakini utafiti uliongozwa na Taasisi ya Maendeleo ya Nchi za Nje ya Uingereza (ODI) umegundua kwamba mataifa hayo yanatumia takriban dola bilioni 100 kila mwaka kuendeleza utumiaji wa nishati asilia nchini mwao na nje ya nchi zao katika mwaka 2015 na 2016.
"Licha ya kundi la G7 kuahidi kupunguza utumiaji wa nishati asilia, lakini hawana mfumo wowote wa kuhakikisha uwajibikaji wa kutimiza ahadi hiyo - na hawana muongozo au miango yoyote," amesema Shelagh Whitley, mmoja wa waandishi wa ripoti hiyo, akizungumza na shirika la habari la Reuters.
Watafiti wa ripoti hiyo wametengeneza orodha ya kila nchi na jinsi inavyoelekea kuachana na utumiaji wa nishati hizo asilia.
Ufaransa inaongoza kwa kupata alama 63 kati ya 100, ikifuatiwa na Ujerumani iliyopata alama 62, Canada ni ya tatu kwa kupata alama 54 na Uingereza imepata alama 47.
Marekani inashika mkia kwa kupata alama 42 kati ya 100, kutokana na kwamba nchi hiyo inaunga mkono utumiaji wa nishati asilia na ilijitoa kutoka katika makubaliano ya kimataifa ya kupambana na kitisho cha mabadiliko ya tabianchi.
Rais wa Marekani Donald Trump alitangaza mwaka mmoja uliopita kujitoa katika makubaliano hayo yaliyoafikiwa na takriban nchi 200.
Wawekezaji wahimiza mataifa ya G7 kupambana na mabadiliko ya tabianchi
Wakati huo huo, makampuni kadhaa makubwa ya uwekezaji, ikiwamo kampuni ya Ujerumani ya Allianz Global Investors, yamewahimiza viongozi wa mataifa hayo saba yaliyostawi zaidi kiviwanda (G7) kuongeza juhudi za kupambana na suala la mabadiliko ya tabianchi na kutimiza ahadi ya kupunguza uzalishaji wa gesi chafu kwa kuachana kabisa na utumiaji wa makaa ya mawe.
Kundi la wawekezaji wapatao 288 limesema katika taarifa yake, kwamba mabadiliko ya utumiaji wa nishati safi yapo njiani, lakini serikali zinahitaji kuongeza juhudi. Hata hivyo wito huo wa wawekezaji unategemewa kupuuzwa na Marekani. Rais Donald Trump amesema wazi kwamba angependa kuiimarisha sekta ya nishati ya makaa ya mawe na gesi, na kuonyesha mashaka juu ya utafiti wa kisayansi wa mabadiliko ya tabia nchi.
Mwandishi: Yusra Buwayhid/rtre/DW
Mhariri: Iddi Ssessanga