Somalia na Ethiopia zafanya mazungumzo nchini Uturuki
2 Julai 2024Nchi mbili ambazo ni hasimu katika Pembe ya Afrika za Somalia na Ethiopia, jana zilifanya mazungumzo nchini Uturuki katika juhudi za kutuliza mivutano inayozidi kuongezeka kufuatia makubaliano yaliyofikiwa baina ya Addis Ababa na Somaliland.
Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Hakan Fidan, amewaeleza waandishi wa habari mjini Ankara kwamba, nchi hizo mbili zimekubaliana kuendeleza mazungumzo kwa nia ya kutatua masuala yanayozozaniwa na utulivu wa kikanda. Mzozo waifanya Somalia kutishia kuwatimua wanajeshi wa Ethiopia
Chini ya mkataba huo uliosainiwa mwanzoni mwa mwaka huu, Somaliland ilikubali kukodisha eneo la kilomita 20 la pwani yake kwa miaka 50 kwa Ethiopia, ambayo inataka kuanzisha kituo cha jeshi la majini na bandari ya kibiashara.
Kwa upande wake, Somaliland ambayo ilijitangazia uhuru wake kutoka Somalia mwaka 1991, imesema Ethiopia itaitambua rasmi, ingawa madai haya hayajathibitishwa na Addis Ababa.