NCCR-Mageuzi yaionya CCM
19 Februari 2020Onyo hilo limetolewa katika mkutano wa NCCR-Mageuzi uliofanyika Dar es Salaam hii leo wakati Watanzania wakiendelea kushuhudia vuguvugu la wananchama na wafuasi wa vyama vya upinzani kuvihama vyama vyao na kujiunga na chama tawala CCM huku wote wakiwa na hoja ya kuunga mkono juhudi za maendeleo za rais John magufuli.
Katika mkutano wa halmashauri kuu ya chama cha NCCR-Mageuzi uliofanyika leo, wajumbe wamezungumzia wasiwasi wao kwa serikali iliyoko mamlakani chini ya chama tawala CCM, wakionya kuwa changamoto za kidemokrasia zinazojitokeza katika awamu hii ni mpango wa kuirudisha Tanzania katika mfumo wa chama kimoja, jambo ambalo wamesema ni kinyume na matakwa ya wa Tanzania wengi wanaohitaji fikra mbadala.
Mbatia asema hana mpango wa kuhamia CCM
James Mbatia mwenyekiti wa chama hicho ameuambia mkutano kuwa hawezi kuhamia chama tawala CCM sababu yeye ni muumini wa demokrasia na ameshiriki katika gharama za kujenga mfumo wa vyama vingi uliorejeshwa takriban miongo miwili sasa
Mkutano huo uliobeba kauli mbiu ya "Utu, umoja pamoja tutashinda" unafanyika katika kipindi ambacho taifa hilo la Afrika mashariki linakabiliwa na hali ngumu ya kisiasa ikiwemo uhaba wa usawa katika uendeshaji wa shughuli za kisiasa, madai ya tume huru ya uchaguzi pamoja na kutawala kwa hofu ya kujieleza.
Akizungumzia hoja kuu ya kuua mfumo wa vyama vingi nchini humo, aliyekuwa mwanachama na mgombea wa jimbo la Busokelo kupitia chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA) ambaye hii leo amehamia katika chama hicho Boniphas Mwabukusi amesema, endapo taifa litafanikiwa kuua mfumo wa vyama vingi kitakachofuata ni kuzalisha ugaidi na watu kujieleza kwa namna ya tofauti.
Mkutano huo ambao uliwaalika baadhi ya wanasiasa kutoka vyama vingine vya upinzani utahitimishwa kwa kutolewa na kujadili maazimio ambayo chama hicho kinasema yatakuwa dira yake kuelekea uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu.