Navalny afariki dunia gerezani Urusi
16 Februari 2024Idara ya Magereza ya Urusi ilisema Navalny alijihisi mgonjwa baada ya matembezi asubuhi ya Ijumaa (Februari 16) na kupoteza fahamu.
Idara hiyo iliongeza kuwa juhudi za kumpatia matibabu ya dharura hazikufanikiwa na akafariki dunia.
Navalny alikuwa akitumikia kifungo cha zaidi ya miaka 30.
Soma zaidi: Urusi yamkamata mkosoaji mwingine wa Kremlin
Msemaji wa Ikulu ya Kremlin, Dmitry Peskov, alisema Rais Vladimir Putin tayari alikuwa amejulishwa kuhusu kifo hicho na kwamba ni jukumu la madaktari kufafanua sababu yake.
Ofisi yake haijajulishwa
Hata hivyo, katibu wa habari wa Navalny, Kira Yarmysh, alisema yeye na timu yake hawajafahamishwa kuhusu kifo hicho cha Navalny.
Kamati ya Uchunguzi ya Urusi imesema imeanzisha uchunguzi kuhusu kifo hicho.
Soma zaidi: Kiongozi wa upinzani Urusi Alexei Navalny ahukumiwa miaka mingine 19 jela
Viongozi wa ulimwengu wanaendelea kutuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Navalny wakisema Rais Putin anapaswa kuwajibishwa kufuatia kifo hicho.
Nchi za Magharibi zinasema mwanasiasa huyo aliyatoa muhanga maisha yake ili kupigania demokrasia na uongozi bora.