Guterres aitaka China kuruhusu Mkuu wa Haki kuzuru Xinjiang
5 Februari 2022Guterres amekutana na Rais Xi Jinping wa China na waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Wang Yi pembezoni mwa michezo ya Olimpiki ya majira ya baridi mjini Beijing.
Soma zaidi: Michezo ya Olimpiki msimu wa baradi yaanza rasmi Beijing
Tangazo kutoka mkutano wa viongozi hao limesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa '' ameelezea matumaini yake kwamba mawasiliano kati ya ofisi ya Kamishna wa Haki za Binadamu na maafisa wa serikali ya China, yataruhusu ziara 'yenye kuaminika' ya kamishna huyo nchini China, ikiwa ni pamoja na jimbo la Xinjiang.''
Taarifa ya shirika la habari la serikali ya China, Xinhua kuhusu mkutano huo na Guterres, haikusema chochote kuhusu suala hilo la haki za binadamu.
Shutuma nzito za wanaharakati
Watetezi wa haki za binadamu wanasema kuwa watu wasiopungua milioni moja kutoka jamii ya Waislamu walio wachache, wamelazimishwa kuishi katika ''kambi za mafunzo'' jimboni Xinjiang lililo magharibi mwa China, wakiituhumu China kwa uhalifu mkubwa wa haki za binadamu, unaohusisha kuwafunga kizazi wanawake wa jamii hiyo, na kazi za shuruti.
Soma zaidi: China yamulikwa kwa ukiukaji wa haki za binaadamu
Mnamo siku zilizotanguliwa kufunguliwa rasmi kwa michezo ya Olimpiki ya majira ya baridi mjini Beijing, wizara ya mambo ya nje ya China ilisisitiza katika mikutano yake ya kila siku na waandishi wa habari, kuwa Guterres anaiunga mkono michezo hiyo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa binafsi amempongeza rais Xi kwa kuiandaa michezo hiyo walipokutana mjini Beijing, imeeleza taarifa ya Umoja wa Mataifa.
Hata hivyo, hadi sasa China imemzuia Michelle Bachelet ambaye ni rais wa zamani wa Chile, kufanya ziara iliyo huru katika jimbo la Xinjiang.
China yakanusha kufanya 'mauaji ya halaiki' Xinjiang
Serikali ya Marekani pamoja na mabunge ya nchi nyingine tano za magharibi, wametangaza kuwa inachokifanya China dhidi ya watu wa jamii ya Uyghurs jimboni Xinjiang ni sawa na ''mauaji ya kuangamiza'', tuhuma ambazo China inazikanusha vikali.
Soma zaidi: Rais Vladmir Putin amewasili mjini Beijing.
China vile vile imewaonya wakosoaji wake kuacha kuitumia michezo ya Olimpiki kwa malengo ya kisiasa. Tayari michezo hiyo inafunikiwa na viwingu vya ukiukaji wa haki za binadamu, Covid-19, na hofu juu ya kinachoweza kutokea kwa wanariadha wtakaotoa mawazo yao wakishiriki katika michezo hiyo.
Kwenye sherehe za ufunguzi, China ilimchagua mwanariadha chipukizi kutoka jamii ya Uyghur Dinigeer Yilamujiang kuwa miongoni mwa watu walioukimbiza mwenye wa michezo hiyo, hatua ambayo bila shaka ilikuwa na ujumbe wa wazi kisiasa.
Ripoti ya Umoja wa Mataifa yacheleweshwa
Wanaharakati na wanasiasa wamekuwa wakisubiri kwa hamu ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu jimboni Xinjiang, kwa matumaini kuwa ingechapishwa kabla ya michezo ya Olimpiki kuanza, lakini mwezi uliopita umoja huo ulisema bayana kuwa isingetangazwa kabla ya michezo hiyo.
Gazeti la South China Morning Post linaloandikwa mjini Hong Kong liliashiria kuwa China ilikubali kuridhia ziara ya Michelle Bachelet, kwa sharti kuwa Umoja wa Mataifa ucheleweshe uchapishaji wa ripoti hiyo ya hali ya haki za binadamu.
afpe