1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUbelgiji

NATO yaunga mkono ujumbe wa mafunzo na msaada kwa Ukraine

13 Juni 2024

Mawaziri wa ulinzi wa jumuiya ya kujihami ya NATO wanakutana mjini Brussels Alhamisi na Ijumaa kwa siku mbili za mazungumzo ili kukubaliana kuhusu ujumbe wa msaada wa mafunzo kwa Ukraine.

https://p.dw.com/p/4gz4w
Mawaziri wa ulinzi wa jumuiya ya NATO wakutana Brussels, Ubelgiji
Mawaziri wa ulinzi wa jumuiya ya NATO wakutana Brussels, UbelgijiPicha: Dursun Aydemir/Anadolu/picture alliance

Akizungumza leo Alhamisi katika kikao cha waandishi habari kabla ya mkutano huo, Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg amewahimiza washirika kuidhinisha mpango wa NATO kusimamia uratibu wa msaada wa usalama na mafunzo kwa Ukraine.

Mradi huo ni sehemu muhimu ya mpango wa bajeti wa ulinzi kwa Ukraine ambao muungano huo wa kijeshi wenye nchi 32 wanachama unataka kuidhinisha katika mkutano wa kilele wa NATO mjini Washington mwezi Julai.

Lengo ni kukabidhi jukumu la uratibu wa msaada wa kijeshi kwa Ukraine kutoka kwenye muundo usio rasmi, unaoongozwa na Marekani unaofahamika kama Kikundi cha Mawasiliano cha Ulinzi wa Ukraine kwa miundo rasmi ya NATO.