1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO yatilia mashaka uondoaji zaidi wa askari wa Urusi

16 Februari 2022

Urusi inaendelea kuwaondoa wanajeshi wake karibu na mpaka wa Ukraine kufuatia kukamilika kwa luteka za kijeshi. Ukraine na nchi za Magharibi hata hivyo zimesema ni vigumu kuyaamini madai hayo ya Urusi.

https://p.dw.com/p/475uW
Russland | Militärfahrzeuge werden nach Ende von Militärübungen auf Züge geladen
Picha: Russian Defense Ministry Press Service/AP/picture alliance

Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema vikosi kadhaa vilivyohusika katika mazoezi ya rasi ya Bahari Nyeusi ya Crimea, ambayo Urusi iliichukua kimabavu kutoka Ukraine mwaka wa 2014, sasa vimerejea makambini.

Soma zaidi: Scholz akutana na Putin, Urusi yaondosha wanajeshi mpakani

Shirika la habari la serikali Ria Novosti lilitoa video ikionyesha msafara wa vifaru na magari mengine ya kijeshi yakisafiri gizani kwenye daraja la Crimea linalounganisha rasi hiyo na Urusi. Wizara ya ulinzi haikutoa maelezo zaidi kuhusu aina ya wanajeshi walioondolewa na idadi ya askari waliohusika.

NATO-Russland Rat tagt in Brüssel
NATO inasema hakuna ushahidi kuwa askari wa Urusi wamepungua mpakani UkrainePicha: Alexey Vitvitsky/Sputnik/picture alliance/dpa

Hatua hiyo inaleta matumaini madogo kuwa mzozo huo kwenye mpaka wa Ukraine unapungua baada ya wiki kadhaa za shughuli lukuki za kidiplomasia na vitisho kutoka kwa nchi za Magharibi vya kutangaza vikwazo vikali kama Urusi itaivamia Ukraine. Lakini mashaka kuhusu nia ya Moscow bado ni makubwa. Ukraine, Marekani, madola ya Ulaya na Jumuiya ya Kujihami ya NATO wote wamedokeza kuwa hawawezi kuiamiamini Urusi moja kwa moja kwa inachosema na kuwa wanahitaji uthibitisho huru.

Soma pia:Marekani inatarajia nini kutoka Ujerumani katika mzozo wa Ukraine?

Rais wa Halmashauri Kuu ya Ulaya Ursula von der Leyen amesema leo kuwa Urusi bado inahitaji kuthibitisha kuwa iko tayari kuutuliza mzozo.

Von der Leyen amewaambia wabunge wa Ulaya kuwa Moscow inatuma ishara zinazokinzana, akimaanisha masharti ya Bunge la Urusi ya kuyatambua majimbo ya mashariki mwa Ukraine ya Donetsk na Luhansk pamoja na kauli ya mkuu wa NATO Jens Stoltenberg iliyosema bado hawajaona ushahidi wa kupungua vikosi vya Urusi mpakani.

Ukraine I Präsident Volodymyr Zelensky
Rais Zelensky ametangaza siku ya Umoja UkrainePicha: Ukrainian Presidential Press/AP/picture alliance

Mjini Brussels, mawaziri wa ulinzi wa nchi 30 wanachama wa NATO – akiwemo Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin – baadaye leo watajadili mipango ya hatua Zaidi za kuizuia Urusi dhidi ya kuivamia Ukraine.

Washirika wa NATO wamekuwa wakipeleka manowari zaidi, ndege za kivita na askari mashariki mwa Ulaya na kuwaweka wanajeshi wengine katika hali ya kuwa tayari kutumwa vitani.

Soma pia: Urusi yaanza kuondoa wanajeshi wake Ukraine

Wakati huo huo, Ukraine inaadhimisha leo kile imekiita "siku ya umoja”. Rais Volodymyr Zelensky aliitangaza siku hiyo mapema wiki hii baada ya ripoti katika vyombo vya Habari vya Marekani kutaja Februari 16 kuwa siku ambayo Urusi ingefanya uvamizi.

Waukraine walipeperusha bendera za taifa na kucheza wimbo wa taifa kuonyesha umoja dhidi ya kitisho cha uvamizi wa Urusi. Rangi za taifa za njano na bluu zilishamiri kila mahali kuanzia shuleni, hospitalini hadi nje ya maduka.

dpa, reuters, ap, afp