NATO yajiandaa kuongeza wanajeshi na silaha Ulaya Mashariki
29 Juni 2022Mjini Madrid nchini Uhispania,viongozi wa Jumuiya ya NATO wamelaani kile walichokiita vitendo vya ukatili vinavyofanywa na Urusi nchini Ukraine na kuahidi kuipatia msaada zaidi serikali ya mjini Kiev wakati ambapo nchi hiyo inakabiliwa na mashambulizi kutoka Moscow.
Mkutano wa Madrid umeanza kwa tamko la katibu mkuu wa Jumuiya hiyo ya NATO aliyewakaribisha viongozi wote na kuzialika pia Sweden na Finland kujiunga kwenye umoja huo.Katibu mkuu Jens Stoltenberg ameitaka Ukraine kuweka matumaini na Jumuiya kwa kutambua iko pamoja na nchi hiyo wakati wote.
Mkuu huyo wa NATO hakuchelea kutangaza kwamba Urusi ni kitisho kikubwa na cha moja kwa moja kwa amani na usalama wa wanachama wote wa jumuiya hiyo.Lakini pia Jens Stoltenberg katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano huo amefafanua umuhimu wa mkutano huu wa kilele kwa kusema.
"Mkutano huu wa kilele utafanya maamuzi muhimu ya kuiimarisha jumuiya ya NATO katika ulimwengu wenye hatari zaidi na ushindani,ambako tawala za kimabavu kama Urusi na China zinapinga waziwazi sheria zinazozingatia utaratibu wa kimataifa.''
Suala kubwa linalotamalaki ajenda za mkutano huu wa kilele ni mgogoro wa Ukraine ambao jumuiya hiyo unautazama kama mgogoro mkubwa kabisa wa kiusalama uliowahi kutokea tangu kumalizika vita vya pili vya dunia.
Kadhalika jumuiya hiyo imeahidi kuongeza hatua za kisiasa na msaada wa moja kwa moja kwa Ukraine kuukabili uvamizi wa Urusi.Ingawa rais Volodymyr Zelensky aliyepewa nafasi ya kuhutubia mkutano huo leo Jumatano ameikosoa Jumuiya hiyo kwa kushindwa kuikumbatia zaidi na kuisadia kikamilifu nchi yake inayohangaika kupambana.
Zelensky ameomba msaada zaidi wa silaha lakini pia juu ya msaada huo ametaka Ukraine isaidiwe kiuchumi kwa kupatiwa fedha zaidi.
"Msaada wa fedha kwa Ukraine ni muhimu kama ilivyo msaada wa silaha .Urusi bado inapokea mabilioni kila siku na kuzitumia kwenye vita.Sisi tuna nakisi ya mabilioni ,hatuna mafuta hatuna gesi ambavyo vingetusadia kuziba pengo hilo.Tunahitaji kiasi dola bilioni 5 kila mwezi,hilo mnalijua''
Zelenskyy pia ameonesha kulalamika kuhusu kukaribishwa Sweden na Finland kwenye mfungamano huo akisema jumuiya hiyo ya NATO haikuonesha sera ya kuacha milango wazi kwa nchi yake kama ilivyofanya kwa nchi hizo mbili.
Jumuiya ya NATO inajiandaa kufanya maamuzi makubwa ikiwemo kuongeza wanajeshi na silaha watakaopelekwa Ulaya mashariki.Hatua hiyo inachukuliwa kwa mara ya kwanza tangu vilipomalizika vita baridi.
Katibu mkuu Jens Stoltenberg amesema vita vilivyoanzishwa na rais Vladmir Putin dhidi ya Ukraine vimeiondowa amani barani Ulaya na kutengeneza mgogoro mkubwa wa kiusalama katika bara hilo.
Viongozi wa jumuiya hiyo ya wanachama 30 pia wanatarajiwa kutangaza mkakati mpya wa jumuiya hiyo utakaoweka wazi vipaumbele na malengo yao yakuzingatiwa katika kipindi cha muongo mmoja.Tukumbushe mkutano huo kwa mara ya kwanza zimealikwa Japan, Australia, Korea Kusini na New Zealand zinazoshiriki kama wageni na kuonesha umuhimu unaoongezeka wa eneo hilo la Asia na Pasifiki.