1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NATO, Marekani zatafautiana kuondosha wanajeshi Afghanistan

18 Novemba 2020

Wakati Marekani ikitangaza rasmi kuondosha idadi kubwa ya wanajeshi wake Iraq na Afghanistan, mkuu wa Shirika la NATO, Jens Stoltenberg, ameonya hatua hiyo inaweza kuigeuza Afghanistan kuwa "jukwaa la magaidi".

https://p.dw.com/p/3lT5y
NATO Generalsekretär Jens Stoltenberg
Picha: Getty Images/AFP/M. Kappeler

Kauli ya Stoltenberg ilitolewa jana muda mchache kabla ya wizara ya ulinzi ya Marekani kutangaza kwamba itapunguza kwa kiasi kikubwa wanajeshi wake nchini Afghanistan, ambako wanasaidiana na kikosi cha NATO, na pia Iraq na kubakisha wachache sana baada ya takribani miaka 20 ya vita. 

Katibu mkuu huyo wa NATO alisema kundi la kigaidi ya ISIS linaweza haraka kurejesha dola ililolipoteza Iraq na Syria kwenye ardhi ya Afghanistan, endapo Marekani itaondosha wanajeshi wake bila mipango inayowashirikisha wengine.

Hilo ni tamko la nadra kwa mkuu huyo wa NATO, ambaye kawaida huwa hamkosoi hadharani Rais Trump wa Marekani, ambaye ndiye aliyechukuwa uamuzi huo.

Hapo jana, kaimu waziri wa ulinzi wa Marekani, Christopher Miller, aliwaambia waandishi wa habari kwenye makao makuu ya jeshi, Pentagon, kwamba wanajeshi 2,000 wataondoshwa nchini Afghanistan kufikia tarehe 15 mwezi Januari mwakani, huku wengine 500 wakirejeshwa kutoka Iraq, na hivyo kubakisha wanajeshi 2,500 tu kwa kila nchi.

Marekani yaazimia kuondoka Iraq na Afghanistan

Hata hivyo, Miller alisema kwamba alishalizungumza suala hilo na washirika wa Marekani kwenye jumuiya ya NATO na pia Rais Ashraf Ghani wa Afghanistan:

USA Washington | Christopher Miller, kommissarischer Verteidigungsminister
Kaimu Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Christopher Miller.Picha: Manuel Balce Ceneta/AP Photo/picture alliance

"Tuliingia pamoja, tunarekebisha pamoja na muda ukifika, tutaondoka pamoja. Hili linakwendana na mipango yetu ya awali na malengo ya kimkakati, inayoungwa mkono na watu wa Marekani na halihusiani na mabadiliko kwenye sera ya Marekani wala malengo yake." Alisema Miller.

Marekani ina wanajeshi wapatao 4,500 nchini Afghanistan na 3,000 nchini Iraq. Muda mchache baada ya tangazo lake hilo la kuondowa wanajeshi jana, kulitokea mashambulizi ya maroketi yaliyoelekezwa kwenye ubalozi wake mjini Baghdad, Iraq, ingawa hakukuwa na taarifa za madhara ndani ya ubalozi wenyewe.

Uamuzi huu wa utawala wa Trump - unaomalizika muda wake tarehe 20 Januari mwakani - huenda ukayachukiza makundi ya wapiganaji kote Afghanistan na Iraq, ambao kwa muda mrefu yamekuwa yakiitaka Marekani iondoshe wanajeshi wake wote mara moja. 

Katika tamko lake, Stoltenberg alirejea kile ambacho pia kimekuwa msimamo wa muda mrefu wa NATO, kwamba vikosi vya jumuiya nchini Afghanistan "vinaendelea kwenye uangalizi na kwamba wataondoka tu pale ambapo muda wa kufanya hivyo umewadia" na kwamba wanajeshi wote wataondoka pamoja kwa njia iliyoratibiwa vyema.

Kwa mujibu wa katibu mkuu huyo wa NATO, hivi saa kuna wanajeshi 12,000 wa NATO nchini Afghanistan, ambapo zaidi ya nusu ni wanajeshi wasio Wamarekani, na ambao mipango ya awali ilikuwa ni kuwaweka hadi mwaka 2024 kwa ajili ya kuvipa mafunzo vikosi vya usalama vya Afghanistan.