Nani akabidhiwe wadhifa gani katika Umoja wa Ulaya
28 Mei 2019Rais wa baraza la Ulaya, Donald Tusk na mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa ulaya Jean-Claude Juncker ndio watakaofungua majadiliano hayo wakati wa mkutano wa dharura wa kilele ulioitishwa kutathmini zahma iliyosabishwa na uchaguzi wa bunge la Ulaya. Watahitaji muda wa chini ya mwezi mmoja kufikia maridhiano pamoja na bunge, kabla ya mkutano wa kilele utakaoitishwa Juni 20 na 21 inayokuja.
"Kinyang'anyiro cha kuania mataji" kitaanza ili kujua nani akabidhiwe wadhifa gani" alisema hapo awali mmojawapo wa wagombea kiti cha mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya, Frans Timmermans, ambae ndie anaeongoza kundi la vyama vya kisoshialisti katika bunge la Ulaya.
Mabishano makali yanatarajiwa. Wafuasi wa vyama vya kihafidhinha vinavyounga mkono Umoja wa Ulaya EPP wanadai mgombea wao Manfred Weber ndie anaestahiki kukabidhiwa wadhifa wa mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya.
Mabishano juu ya nani akabidhiwe wadhifa wa mwenyekiti wa halmashauri kuu
Chama hicho cha kihafidhina kinaendelea kukalia wingi wa viti katika bunge la Ulaya licha ya kupoteza zaidi ya viti 30 ikilinganishwa na uchaguzi wa mwaka 2014. Na madai yake ya kukabidhiwa wadhifa wa mwenyekiti hayaungwi mkono na viongozi wote wa Umoja wa ulaya. Wanapanga kumtanabahisha aachane na madai hayo ili kuepukana na mzozo. Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron anapinga wazo la kwamba mwenye kuongoza orodha ya wagombea ndie anaebidi akabidhiwe wadhifa huo. Emmanuel Macron anapanga kukutana pamoja na viongozi wengine wa Umoja wa Ulaya ikiwa ni pamoja na kansela Angela Merkel kuzungumzia utata huo kabla ya mkutano wa kilele kuanza.
Na wakuu wa makundi ya vyama vinavyowakilishwa katika bunge la Ulaya nao pia wanapanfga kukutana wakati woweote kutoka sasa.
Wadhifa wa mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya ni miongoni mwa zile nyadhifa zinazohitaji kukabidhiwa viongozi wepya, sawa na ule wa rais wa baraza la Ulaya, mwakilishi mkuu wa siasa ya nje na mkuu wa benki kuu ya Umoja wa Ulaya.
Viongozi wa Umoja wa Ulaya ndio wanaomteuwa mwenyekiti wa halmashauri kuu lakini anabidi aidhinishwe na bunge la Ulaya.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/dpa/AFP
Mhariri: Sekione Kitojo