Nane bora zajulikana
2 Julai 2014Mechi ya kwanza ilikuwa kati ya Argentina na Uswisi ambayo mwanzoni haikuwa na ufundi wa kuridhisha, kinyume na ilivyotarajiwa. Kikosi cha Uswisi ambacho mwanzoni hakikupewa nafasi kubwa, kiliwashangaza wengi kwa kubururana na Argentina hadi dakika za nyongeza, baada ya kipindi cha kawaida kumalizika matokeo yakiwa bado sufuri kwa sufuri. Kitendawili kiliteguka zikisalia dakika tatu tu hadi mikwaju ya penalti, pale nahodha wa Argentina Lionel Messi alipoitumia nafasi ya nadra iliyopatikana, na kumtengea Ange di Maria ambaye bila ajizi aliumimina mpira wavuni, na kumuacha mlinda mlango wa Uswisi Diego Benaglio akiduwaa baada ya kazi kubwa ya karibu saa mbili za mchezo.
Mnamo dakika za lala salama Uswisi ilitumia kila ilicho nacho kutaka kusawazisha, na karibu juhudi zao zingezaa matunda mwishoni mwishoni pale kombora la kichwa lililorushwa na Blerim Dzemaili lilipoubamiza mwamba na kumrudia, lakini aliporudisha mpira ukalikosakosa lango kwa sentimita chache. Uswizi iliponea chupuchupu kubugizwa bao la pili, pale yule yule Ange Di Maria alipojaribu bahati yake na kuurusha mkwaju wa mbali kuelekea lango lao lililoachwa wazi, baada ya kipa wa Uswisi kujiunga na pilika pilika za kusaka goli la kusawazisha.
Hadi kipenga cha mwisho, Argentina 1, Uswisi 0. Kocha mkongwe wa Uswisi Ottmar Hitzfeld alitangaza pale pale kustaafu, kama alivyokuwa ameahidi mwanzoni mwa mashindano haya.
Mkimbizano kati ya Marekani na Ubelgiji
Mechi iliyofuata kati ya Marekani na Ubelgiji pia haikuanza kwa msisimko, lakini ilimalizika kwa mtindo kwa kasi kubwa na kila aina ya msisimko.
Ubelgiji ambayo haikuweza kuliona lango la Marekani katika muda wa kawaida licha ya fursa chungu nzima, ilianza kipindi cha nyongeza kwa kishindo pale Kevin de Bruyne alipokamilisha mashambulizi yaliyoanzishwa na Romelu Lukaka, na kuuvunja ukaidi wa golikipa wa Marekani ambaye aling'ara kwa kuokoa mikwaju mingi zaidi tangu kuanza mashindano haya.
Marekani hawakukubali kunyosha mikono. Juhudi za pamoja za Geoff Cameron, Graham Zusi na Clint Dempsey ziliendelea kuitia shinikizo ngome ya Ubelgiji, ambayo ilijizatiti chini ya nahodha Vincent Kompany. Mchezo ulionekana kupata mwelekeo pale Romelu Lukaku aliyeingia katika kipindi cha nyongeza akichukua nafasi ya chipukizi Divock Origi, alipopachika bao la pili baada ya wamarekani kuisahau safu yao ya ulinzi, na kujikita kwenye mashambulizi.
Wamarekani waonyesha matumaini
Wamarekani hawakukata tamaa bali waliendelea kuirusha mipira mbele, huku wakiwa hawana cha kupoteza tena katika mechi ambayo walijitolea kwa kila hali. Michael Bradley alirusha mkwaju uliounganishwa vyema na Julian Green ambaye pia aliingia kutoka benchi, na kufyatua fataki lililompita kipa Curtois, zikisalia dakika 2 tu kutimia dakika 120.
Hadi hapo bado wamarekani walikuwa bado hawajasalimu amri, na Jermain Jones nusra augeuze mchezo kichwa chini miguu juu, lakini shuti lake liliambaaambaa likipita kando ya langu na kutoa ahueni kwa wabelgiji. Baada ya kipenga cha mwisho wachezaji wa timu mbili na makocha wao walipongezana kwa kazi nzuri waliyofanya, na licha ya kushindwa, wamarekani walishangiliwa vikali na mashabiki wao waliojaa uwanja.
Sura ya robo fainali sasa ni kama ifuatavyo,Ijumaa saa moja usiku huko Afrika Mashariki, Ufaransa itajitosa uwanjani dhidi ya Ujerumani, na baadaye saa tano usiku, wenyeji Brazil watashuka dimbani na Colombia. Kesho yake, yaani Jumamosi, Argentina wanayo miadi na Ubelgiji saa moja usiku, na mechi ya kukamilisha ratiba itakuwa kati ya Uholanzi na Kosta Rica, saa tano usiku jumamosi hiyo hiyo.
Mwandishi: Daniel Gakuba/RTRE/APE
Mhariri: Iddi Ssessanga