Mzozo wa Libya wajadaliwa mjini Geneva
15 Januari 2015Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa Leon Bernardino amesema mchakato wa kuyafikia makubaliano ya amani ya Libya utakuwa mgumu na mrefu. Bernardino ambaye anayasimamia mazungumzo hayo mjini Geneva nchini Uswisi amekiri hawatarajii kufikia muafaka leo wala kesho, kwa sababu kuna pengo kubwa kati ya makundi ya Libya, ambalo linazidi kutanuka kutokana na mapigano yanayoendelea nchini humo.
Bernardino aidha amesema mazungumzo hayo yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa yanalenga kufikia suluhisho la kisiasa na makubaliano ya kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa, ambapo Walibya wote watawakilishwa. Serikali hiyo itachukua nafasi ya tawala zinazopingana, ambazo vita vyao vya kung'ang'ania madaraka vimesababisha vifo vya mamia kadhaa ya watu katika kipindi cha miezi sita iliyopita.
Mazungumzo ya Geneva yananuia kufikia makubaliano kuhusu mbinu za kuyakomesha kabisa mapigano na kuhakikisha makundi yote yenye silaha yanaondoka kutoka miji mikubwa. Bernardino amesema, "Ni muhimu sana kwamba suluhisho lolote litakalofikiwa katika mazungumzo haya liungwe mkono kwa dhati na watu wa Libya. Sidhani kama kutakuwa na haja kwa serikali ya mpito inayotakiwa kuikwamua nchi kutokana na machafuko kuandaa kura ya maoni. Kuna mapigano yanayoendelea na hali ni ngumu. Huwezi kuandaa kura ya maoni wala uchaguzi kukiwa na machafuko."
Mkutano wa Geneva ulitarajiwa kuwaleta pamoja wajumbe wa serikali iliyojitangazia madaraka ambayo iliudhibiti mji mkuu Tripoli mwaka uliopita, pamoja na serikali inayotambuliwa kimataifa ya waziri mkuu Abdullah al-Thini, na makundi ya waasi yanayoziunga mkono serikali hizo mbili. Watawala wa Tripoli walisema bunge leo limeahirisha uamuzi wa kujiunga na mazungumuzo ya Geneva mpaka Jumapili ijayo kwa sababu ya wasiwasi kuhusu jinsi yalivyoandaliwa, hatua inayouweka mchakato mzima mashakani.
Mazungumzo hayatafua dafu
Wachambuzi wameonya kwamba mazungumzo ya Geneva huenda yasiwe na tija yoyote mpaka viongozi wa makundi yaliyojihami na silaha ya Libya, ambao baadhi yao hawashiriki mazungumzo hayo, washirikishwe moja kwa moja. Mchambuzi wa masuala ya kisiasa Mohammed al-Ferjani amesema mdahalo unaoendelea Geneva hautazaa matunda kwa sababu Umoja wa Mataifa haukuchagua washiriki wanaostahiki.
Bernardino amesema mazungumzo haya ya kwanza yanatarajiwa kuendelea hadi kesho Ijumaa na kuanza tena wiki ijayo kama kundi la mjini Tripoli litaamua kuhudhuria, lakini duru zaidi za mazungumzo huenda zikafanyika katika maeneo mbalimbali.
Umoja wa Ulaya umeyaeleza mazungumzo ya Geneva kuwa fursa ya mwisho kuutanzua mzozo wa Libya, ambako serikali mbili zinazopingana na makundi yenye silaha yanalitishia taifa hilo kutumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe, ikiwa ni miaka mitatu tangu kuuwawa kwa aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo hayati Muammar Gaddafi.
Mwandishi:Josephat Charo/AFP/REUTERS
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman