1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa kisiasa Madagascar.

Halima Nyanza/AFP9 Februari 2009

Waziri wa Ulinzi wa Madagascar Cecile Manorohanta leo ametangaza kujiuzulu wadhfa huo, baada ya polisi kuuwa raia 28 waliokuwa wakiandamana kupinga serikali ya nchi hiyo mwishoni mwa wiki, kufuatia mzozo wa kisiasa.

https://p.dw.com/p/Gpy2
Mpinzani wa serikali ya Madagascar, Meya wa mji wa Antananarivo, Andry Rajoelina anasema mapambano bado yanaendelea, kwani watu wanataka mabadiliko nchini Madagascar.Picha: AP

Wakati mapambano ya kugombea madaraka kati ya rais Marc Ravalomanana wa Madagascar na mpinzani wake Andry Rajoelina, yakiongezeka, waziri wa ulinzi wa nchi hiyo Cecile Manorohanta amesema hataki kubakia katika serikali ambayo inalaumiwa kwa kuua raia na kuongeza kuwa akiwa kama mama hawezi kuvumilia ghasia hizo.


Katika taarifa yake iliyotolewa na radio moja binafsi nchini humo, waziri huyo wa ulinzi aliyejiuzulu, ametoa pia salamu za rambirambi kwa familia za wale wote waliokumbwa na maafa hayo katika kipindi hiki ambacho nchi hiyo inakabiliwa na mzozo wa kisiasa.


Amesema ameamua kujitoa serikalini kufuatia kutokea kwa maafa hayo, kwani kama ilivyopitishwa na serikali majeshi ya ulinzi yanapaswa kulinda raia na mali zao, hivyo baada ya kutokea yote hayo ameamua kujiondoa katika serikali hiyo.


Wakati waziri huyo wa ulinzi akitangaza kujiuzulu, kiongozi wa upinzani nchini Madagascar Andry Rajoelina amesema hatosimama na kampeni yake dhidi ya serikali ya nchi hiyo baada ya majeshi ya ulinzi kuua wafuasi wake hao wapatao 28.


Akizungumza wakati alipowatembelea majeruhi waliolazwa hospitalini, mjini Antananarivo, bwana Rajoelina alisema mapambano bado yanaendelea kwani watu wanataka mabadiliko.


Aidha kiongozi huyo wa upinzani ambaye leo anatarajiwa kukutana na msaidizi wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, ametangaza leo kuwa siku ya maombolezo ya kitaifa.


Katika hatua nyingine Umoja wa Mataifa umeitaka serikali ya Madagascar kuwafikisha mbele ya sheria wale wote waliohusika na mauaji ya watu hao walioandamana kuipinga serikali.


Msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ameitaka serikali ya Madagascar kuchukua hatua za haraka ambapo wote waliohusika na mauaji hayo wafikishwe mbele ya sheria.


Jumuiya ya kimataifa na nchi mbalimbali duniani tayari zimetoa kauli zao kuhusiana na mzozo huo wa kisiasa ulioikumba Madagascar, ambapo Ufaransa imelaani ghasia hizo na wale wote wanaosababisha ghasia hizo zinazoongeza mvutano.


Naye rais wa Ujerumani Horst Köhler ambaye alishawahi kuitembelea nchi hiyo, anaielezea hivi Madagascar.

Takriban watu 28 waliuawa na wengine zaidi ya 210 kujeruhiwa baada ya polisi hapo siku ya Jumamosi kuwafyatulia risasi waandamanaji wanaoipinga serikali, katika mji mkuu wa nchi hiyo Antananarivo.