Mzozo wa Israel na Gaza: Mashambulio bado yaendelea
19 Mei 2021Mashambulio hayo ya usiku kucha yamefanyika ikiwa ni siku moja tu baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kumaliza mkutano wake wa dharura kuhusu mzozo huo kati ya Israeli na Gaza bila wanachama wake 15 kufikia makubaliano juu ya tamko la pamoja kuhusiana na muktadha wa juhudi za kidiplomasia zenye lengo la kusimamisha mapigano.
Kwa upande mwingine viongozi wa ulimwengu wanaendelea kuhimiza mapatano kati ya Israeli na kundi la Hamas lakini kutokana na mashambulizi yanayoendelea idadi ya vifo katika mapigano hayo pia inaendelea kuongezeka.
Soma Zaidi:Idadi ya vifo inatajwa kuongezeka Gaza
Ufaransa imesema bado inatafuta uwezekano wa kupatikana azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu kusitishwa kwa mapigano hayo kati ya Israeli na kundi la Hamas,la wapiganaji wa Kipalestina wanaoudhibiti Ukanda wa Gaza.
tofauti na matamko yanayohitaji makubaliano ya wote, maazimio ya baraza la usalama yanawajibisha kisheria.Yanahitaji kura zisizopungua tisa za ndio na pasiwepo kura ya turufu ya kupinga ya mjumbe yeyote wa nchi mwanachama wa kudumu wa baraza hilo. Kulingana na taarifa ya msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric, watu zaidi ya alfu 58 wamegeuka kuwa wakimbizi wa ndani kutokana na mashambulMo ya Israel kwenye Ukanda wa Gaza.
Soma Zaidi:Kwa nini Umoja wa Ulaya hauna ushawishi Mashariki ya Kati?
Jeshi la Israeli limesema lilishambulia maeneo ya wapiganaji wa Hamas karibu na miji ya Khan Younis na Rafah, na ndege zake 52 zilipiga maeneo mengine 40 yaliyo chini ya ardhi kwa muda wa dakika 25. Maafisa wa Israel waliozungumza na shirika la habari la AP wamesema watu sita waliuawa katika mashambulio hayo ya anga yaliyofanyika leo Jumatano.
Wakati huo huo Uturuki imepinga tuhuma za Marekani kwamba Rais Recep Tayyip Erdogan alitoa matamshi ya chuki dhidi ya wayahudi katika kukosoa kwake mashambulio ya Israeli dhidi ya Ukanda wa Gaza. Rais wa Uturuki pia anamlaumu rais wa Marekani Joe Biden kwa kupendelea upande mmoja.
Vyanzo:/AFP/https://p.dw.com/p/3ta71