Mzozo wa Iran na Marekani wahamia nchini Iraq
30 Desemba 2019Wanamgambo hao wamesema watalipiza kisasi kutokana na mashambulio hayo ya uovu yaliyofanywa na kile walichosema ni Wamarekani wasiojitambua.
Shambulio la Marekani , likiwa ni shambulio kubwa kabisa hadi hivi sasa lililolenga wanamgambo wanaoungwa mkono na serikali nchini Iraq , na miito ya kulipiza kisasi, inawakilisha ongezeko jipya la vita vya mataifa mengine vinavvyopiganwa nchini humo kati ya Marekani, na Iran zinazofanya mapambano yao katika mashariki ya kati ambayo yanaweza kutishia maslahi ya Marekani katika eneo hilo.
Miito ya kutaka kulipiza kisasi mjini Baghdad imekuja siku moja baada ya waziri wa ulinzi wa Marekani Mark Esper kusema Marekani imefanya mashambulio hayo ya kijeshi na kulenga wanamgambo wa Iraq wanaoungwa mkono na Iran, ambao inawalaumu kwa shambulio la roketi ambalo lilisababisha kifo cha mkandarasi Mmarekani nchini Iraq wiki iliyopita.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Mike Pompeo amesema mashambulizi hayo yanatuma ujumbe kuwa Marekani haitavumilia hatua zinazofanywa na Iran kuhatarisha maisha ya Wamarekani.
Mashambulizi yaliyopangwa
Jeshi la Marekani lilisema "Mashambulizi yaliyopangwa na kulenga kwa usahihi" yalifanywa dhidi ya maeneo matano ya Kataeb Hezuboullah, ama vikosi vya Hezbollar nchini Iraq na Syria. Kundi hilo, ambalo ni jeshi tofauti kutoka kundi la kijeshi la Hezbollah nchini Lebanon, linafanya shughuli zake chini ya mwamvuli wa wanamgambo wanaoungwa mkono na serikali wanaofahamika kwa jumla kama majeshi ya umma ya kuhamasisha. Wengi wao wanaungwa mkono na Iran.
"Vita vyetu na Wamarekani na mamluki wao sasa vimefunguliwa kwa uwezekano wote," Kataeb Hezbollah limesema katika taarifa usiku wa Jumapili.
"Hatuna chaguo leo mbali ya kupambana na hakuna ambacho kinaweza kutuzuwia kutolipiza kisasi kwa uhalifu huu."
Marekani inawalaumu wanamgambo hao kwa mashambulizi ya maroketi siku ya Ijumaa ambayo yalisababisha mkandarasi wa wizara ya ulinzi ya Marekani katika eneo la kijeshi karibu na Kirkuk, kaskazini mwa Iraq, pamoja na mashambulizi mengine kadhaa katika vituo vya vikosi vya Marekani nchini Iraq ambavyo hakuna kundi lililodai kuhusika nayo.Maafisa wanasema zaidi ya maroketi 30 yalifyatuliwa katika shambulio la Kirkuk.
Msemaji wa kataeb Hezbollah alikana kuwa kundi hilo linahusika na mashambulizi hayo ya maroketi dhidi ya vituo vya Marekani, ikiwa ni pamoja na moja ambalo lilisababisha kifo cha mkandarasi wa Marekani, wakisema Marekani inatumia mashambulizi hayo kama njia ya kulishambulia kundi hilo.