Mzozo mpya waibuka kati ya Pakistan na Iran
18 Januari 2024Pakistan imefanya mashambulizi nchini Iran hii leo, ikiwalenga wanaharakati wanaotaka kujitenga wanaofahamika kama Baloch. Hayo yameelezwa na Wizara ya mambo ya nje ya Pakistan, siku mbili tu baada ya Iran kushambulia ngome za kundi jingine la wanamgambo katika ardhi ya taifa la Pakistan na kusababisha vifo vya watoto wawili kwa mujibu wa serikali mjini Islamabad.
Vyombo vya habari vya Iran vimesema makombora kadhaa yalipiga kijiji kimoja
katika Jimbo la Sistan-Baluchestan ambalo linapakana na Pakistan, na kuua takriban watu tisa. Taarifa za awali zimesema wanawake watatu na watoto wanne waliuawa, na wote wakiwa si raia wa Iran.
Kwa upande wake, wizara ya mambo ya nje ya Pakistan imesema mashambulizi hayo yaliendeshwa kwa ufanisi na usahihi mkubwa na yalilenga maficho ya magaidi na kuwaua kadhaa. Jeshi la nchi hiyo limesema magaidi hao ni kutoka kundi linalojiita "Jeshi la Ukombozi wa Baluchistan".
Soma pia:Iran na Pakistan zatakiwa kujizuia kufuatia shambulio la anga
Wizara hiyo imeendelea kuwa inaheshimu uhuru na mipaka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, lakini ikasisitiza kuwa lengo pekee la kitendo cha leo lilikuwa kulinda usalama na maslahi ya Pakistan, ambayo imesema "ni muhimu na kamwe hayawezi kuathiriwa."
Mvutano wa kidiplomasia kati ya Pakistan na Iran
Pakistan ambayo inamiliki silaha za nyuklia, imemuita nyumbani mwanadiplomasia wake mkuu kutoka Tehran. Mumtaz Zahra Baloch, Msemaji wa Serikali ya Pakistan amesema:
"Tumewafahamisha pia kwamba Pakistan imeamua kumrejesha nyumbani Balozi wake kutoka Iran na kuhusu balozi wa Iran nchini Pakistan ambaye kwa sasa yuko ziarani huko Iran, ni vyema asirudi kwa muda huu."
Aidha, Waziri Mkuu wa muda wa Pakistan Anwaar-ul-haq Kakar amefupisha ziara yake nchini Uswisi ambako alikuwa akihudhuria Kongamano la Kiuchumi duniani huko Davos.
Soma pia: Iran yafanya mashambulizi dhidi ya wanamgambo Pakistan
Mahusiano kati ya majirani hao yamekuwa yakigubikwa mara kadhaa na mivutano, lakini mashambulizi ya hivi punde yanaarifiwa kuwa uvamizi wa hali ya juu zaidi katika miaka ya hivi karibuni.
Mzozo huu kati ya Iran na Pakistan unazidisha wasiwasi wa kuchochea ukosefu wa utulivu katika eneo la Mashariki ya Kati tangu kuibuka kwa mzozo wa Israel na kundi la Hamas. Inahofiwa pia mzozo huo kutanuka zaidi baada ya wanamgambo wenye mafungamano na Iran kutoka Lebanon, Syria, Iraq na Yemen kujitosa katika vita hivyo.
China ambayo ni jirani wa mataifa hayo na mshirika mkuu wa kibiashara imejitolea kuwa mpatanishi katika mzozo huu huku kukiwa na hofu ya kuongezeka kwa mashambulizi zaidi ya kulipiza kisasi. China na Urusi ambazo zina ushawishi eneo hilo zimetoa wito wa kujizuia kwa pande zote mbili na kutoruhusu kuongezeka kwa hali ya migogoro.
(Vyanzo: Mashirika)