Myanmar yawaachia maelfu ya wafungwa katika Siku ya Uhuru
4 Januari 2025Hii ni sehemu ya msamaha uliotolewa kwa watu wengi kwa wakati mmoja katika maadhimisho ya leo ya miaka 77 ya uhuru wa nchi hiyo kutoka kwa Uingereza. Walioachiliwa wanajumuisha idadi ndogo tu ya mamia ya wafungwa wa kisiasa waliotiwa jela kwa kuupinga utawala wa kijeshi tangu jeshi lilipochukua madaraka Februari mwaka 2021 kutoka kwa serikali iliyochaguliwa na wananchi ya Aung San Suu Kyi.
Soma pia: Myanmar yaelezea maendeleo yaliyofikiwa kuelekea uchaguzi wa mwakani
Televisheni ya taifa MRTV imeripoti kuwa Jenerali Mkuu Min Aung Hlaing ambaye ni mkuu wa serikali ya kijeshi, amewapa msamaha wafungwa 5,864 kutoka Myanmar, pamoja na wengine 180 wa kigeni ambao watarudishwa makwao. Kuwachiliwa kwa wafungwa wengi ni jambo la kawaida katika siku kuu za kitaifa na wakati wa matukio mengine muhimu nchini Myanmar.
Katika ripoti nyingine tofauti, Min Aung Hlaing amepunguza hukumu za kifungo cha maisha jela za wafungwa 144 hadi miaka 15 jela. Hakukuwa na dalili kuwa msamaha huo wa kuwaachia wafungwa ungemjumuisha Aung San Suu Kyi, ambaye amekuwa akishikiliwa na jeshi tangu liliponyakua mamlaka. Suu Kyi mwenye umri wa miaka 79 anatumikia kifungo cha miaka 27 baada ya kuhukumiwa kwa mfululizo wa kesi zilizochochwa kisiasa zilizowasilishwa dhidi yake na jeshi.