SiasaMyanmar
Myanmar yatangaza hatua mpya kali dhidi ya 'habari za uongo'
3 Februari 2023Matangazo
Utawala wa Kijeshi nchini Myanmar umeanzisha hatua mpya kali katika ngome za upinzani ambapo watu wanaotuhumiwa kwa uhaini na kueneza habari za uongo watahukumiwa na mahakama za kijeshi.
Hii ni kwa mujibu wa gazeti la serikali ya Myanmar la Global New Light.
Katika miji 37 iliyoathiriwa na hatua hizo, hakuna rufaa itakayoruhusiwa kwa hukumu iliyotolewa na mahakama za kijeshi, isipokuwa kwa hukumu ya kifo, ambayo lazima iidhinishwe na mkuu wa utawala wa kijeshi Aung Hlaing.
Chini ya hatua hizo mpya mahakama za kijeshi zitakuwa na jukumu la kusikiliza kesi za jinai kuanzia uhaini wa juu hadi marufuku ya kueneza habari za uongo, ambayo jeshi limeitumia kuwafunga jela waandishi kadhaa wa habari.