Mwito watolewa wa kurefushwa usitishaji mapigano Sudan
28 Mei 2023Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa mapema leo, Washington na Riyadh zimesema kurefushwa kwa muda wa kuweka chini silaha kutawezesha utoaji wa misaada ya kiutu ya haraka inayohitajika kwa watu wa Sudan.
Mapigano yalizuka nchini Sudan mnamo Aprili 15 kati ya vikosi vya Jeshi la Sudan linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah Al-Burhan na kikosi cha wanamgambo wenye nguvu cha RSF chini ya Jenerali Mohammed Hamdan Dagalo, wakiwania udhibiti wa taifa hilo.
Wiki iliyopita, pande hizo hasimu zilikubaliana kusitisha mapigano kwa muda wa wiki moja, katika makubaliano yaliyosimamiwa na Saudi Arabia pamoja na Marekani.
Licha ya hatua hiyo, kama ilivyokuwa katika makubaliano yaliyopita, mapambano hayakukoma katika mji mkuu Khartoum na kwingineko nchini humo.