Mwisho wa mazungumzo ya nyuklia ya Iran wawadia
24 Novemba 2014Siku ya mwisho iliyowekwa kufikiwa makubaliano ni leo (24 Novemba) lakini China inasema kunaweza kukawa na ulazima wa kurefusha muda. Mwakilishi wa China kwenye mazungumzo hayo anaamini kwamba licha ya pande zote husika kujaribu kufikia kilele cha majadiliano yao hivi leo, wakati unaweza usiwatoshe kufikia makubaliano.
Cheng Jingye, ambaye pia ni mjumbe wa China kwenye Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani, IAEA, aliwaambia waandishi wa habari mjini Vienna kwamba wakati mazungumzo hayo yakiendelea, kumekuwa na masuala mapya yanayozuka, kando ya yale yaliyokuwa yamekusudiwa awali, na hivyo kurefusha vikao vya majadiliano.
"Kumekuwa kukijitokeza mawazo na mapendekezo mapya kwenye mazungumzo haya. Muda wa mwisho wa duru hii ni leo Jumatatu, lakini kwa kuzingatia kwamba baadhi ya masuala ni changamano na muhimu sana, ninadhani muda zaidi unaweza ukahitajika," aliongeza Jingye.
Iran, Marekani zaonesha dalili ya kuongeza muda
Msimamo wa mjumbe huyo wa China unaonekana kuungwa mkono pia na Iran yenyewe. Mapema, afisa mmoja wa Iran kwenye mazungumzo hayo aliliambia Shirika la Habari la Wanafunzi wa Iran (ISNA) kwamba isingeliwezekana kufikia makubaliano ya jumla hivi leo kutokana uchache wa muda na kiwango cha mambo yanayohitaji kujadiliwa kwa undani.
Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, amesema bado kuna tafauti kubwa kati ya pande hizo mbili, ingawa baadhi ya wachambuzi wanaendelea kuwa na matumaini kuwa Iran na mataifa matano yenye kura ya turufu kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na Ujerumani, watafanikiwa hatimaye kusaini makubaliano hayo ya kihistoria ndani ya duru hii ya mazungumzo.
"Tunaweza kuwa na matumaini ya kufikiwa makubaliano. Inawezekana yasipatikane leo tarehe 24 Novemba, lakini nadhani inaonesha kuwa kuna dhamira ya kweli ya kisiasa ya kupatikana, japokuwa huenda tukahitaji nyongeza ya muda kidogo ili kufikia huko kwenye makubaliano," alisema Kelsey Davenport, mchambuzi wa Shirika la Udhibiti wa Silaha Duniani.
Urusi ndio muhimu zaidi kwenye mazungumzo
Kufikia jioni ya jana (23 Novemba), maafisa wa Marekani na Iran walisema walikuwa wameanza mazungumzo juu ya kile wanachokiita Mpango B, ambao unamaanisha kuongeza muda wa majadiliano. Afisa mmoja wa Marekani aliliambia shirika la habari la AFP kwamba ni jambo linalotegemewa kwamba kwa kiwango walichofikia, suala la kuongeza muda linajadilika.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Philip Hammond, alisema pande zote zitajaribu kadiri ziwezavyo kulifikisha suala hili ukingoni Jumatatu. Mwenzake wa China, Wang Yi, aliwasili asubuhi ya Jumatatu mjini Vienna kuungana na wenzake, akiwemo Laurent Fabius wa Ufaransa na Frank-Walter Steinmeier wa Ujerumani na Sergei Lavrov wa Urusi, ambaye anachukuliwa kuwa na uzito sana kwenye mazungumzo haya.
Uingereza, China, Ufaransa, Ujerumani, Urusi na Marekani zilikuwa zimekubaliana na Iran kwamba kufikia saa sita usiku wa leo, tayari ziwe zimeshasaini makubaliano ya jumla ambayo yataiwezesha Iran kuondolewa vikwazo vya miaka 12 vya kiuchumi, ili nayo ipunguze urutubishaji wa madini yake ya uranium, katika kiwango ambacho kamwe hakitafikia uwezo wa kutengeneza silaha za nyuklia.
Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Saumu Yussuf