Mwili wa Malkia Elizabeth II wawasili ukumbi wa Westminster
14 Septemba 2022Jeneza la Malkia Elizabeth II limewasili katika majengo ya bunge ambapo mwili wake utakaa kwa siku nne ili kutoa fursa kwa waombolezaji kutoa heshima zao za mwisho.
Watu nchini Uingereza watapata nafasi adimu ya kutoa heshima zao za mwisho kwa Malkia Elizabeth II katika ukumbi wa Westminster kuanzia saa kumi na moja jioni, majira ya Uingereza leo Jumatano.
Soma pia:Mfalme Charles III aahidi kufuata nyayo za mamake
Hii ni baada ya msafara uliokuwa umeubeba mwili wa Malkia huyo kuwasili kutoka kasri la Buckingham hadi majengo ya bunge.
Milolongo hiyo ya watu imeanza karibu na daraja la Lambeth, wakati maafisa wakisema huenda watu wakaongezeka kufikia hadi ukumbi wa Southwark, kusini mashariki mwa London. Milolongo hiyo ya watu inatarajiwa kuwa mirefu zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini humo.
Mamlaka imepanga kuwepo kwa urefu wa kilomita 16 ya foleni, huku maafisa wa polisi na wasimamizi wa kudhibiti umma wakishika doria. Idadi kubwa ya watu wakiwemo wahubiri na wakalimani wa lugha ya ishara pia wamejitolea kusaidia.
Joan Bucklehurst ambaye ni mmoja wa waombolezaji amesema, "Hii ni historia, Malkia Elizabeth alikuwa na umuhimu mkubwa kwetu. Alikuwa mtu mzuri sana, ndio. Kwa hivyo, ilitubidi tuwe hapa. Tumewahi kuwa hapa mara kadhaa lakini hii ya leo ni hafla maalum, ilikuwa siwezi kukosa."
Malkia Elizabeth II atazikwa katika kanisa maarufu la King George VI
Watu hata hivyo wametahadharishwa kuwa wanaweza kusubiri kwa muda mrefu kuutizama mwili wa Malkia Elizabeth II, japo wamewekwa alama maalum kwenye mikono yao ili waweze kuchukua chakula na kuingia msalani iwapo watahitajika kufanya hivyo, bila ya kupoteza nafasi zao kwenye foleni hiyo.
Watakapofika bungeni, waombolezaji watatakiwa kukaguliwa kwanza. Vitu kama vile rangi ya ukutani, visu, vinywaji, fataki, maua au hata ujumbe wa matangazo umepigwa marufuku kuingia navyo.
Soma pia: Truss amwelezea Malkia Elizabeth kuwa mwanadiplomasia mahiri
Umati huo mkubwa wa watu ni dhihirisho la wazi la mapenzi na heshima waliokuwa nayo kwa Malkia pekee wa karne ya sasa ambao Waingereza wengi wanamfahamu, aliyevuta pumzi zake za mwisho katika kasri la Balmoral nchini Scotland siku ya Alhamisi akiwa na umri wa miaka 96, na kumaliza utawala wake wa miaka 70.
Mfalme Charles III pamoja na familia yake ya kifalme wakiwemo ndugu zake Anne, Andrew na Edward, watatembea nyuma ya msafara utaokuwa umelibeba jeneza la Malkia.
Awali, maelfu ya watu waliokusanyika nje ya kasri la Buckingham kabla ya msafara huo kuanza, walishangilia wakati Charles alipowapungia mkono alipokuwa akielekea katika kasri kutoka katika maakazi yake rasmi ya jumba la Clarence.
Mwili wa Malkia utalazwa katika ukumbi wa Westminster katika majengo ya bunge kwa siku nne kabla ya mazishi yake ya kitaifa mnamo siku ya Jumatatu Septemba 19.
Malkia Elizabeth II atazikwa katika kanisa maarufu la King George VI, karibu na mumewe Philip, majivu ya dada yake binti wa mfalme Margaret, mama yao ambaye pia anaitwa Elizabeth na baba yao, Mfalme George VI.