Mwenyekiti wa CHADEMA Mbowe ana kesi ya kujibu
18 Februari 2022Mbowe pamoja na washtakiwa wengine watatu sasa wataanza kupanda kizimbani kuyakabili mashtaka yao na kulingana na wakili wao, washtakiwa hao wamepanga kuwaleta mahakani hapo mashahidi kadhaa. Uamuzi huo wa mahakama umepokelewa kwa hisia mseto huku chama chake kikisema kitatoa msimamo wake baadaye hii leo.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema upande wa Zanzibar, Salum Mwalimu ameiambia DW kuwa kutokana na ukubwa wa shauri hilo na kwa namna lilivyovutia hisia za wengi, msimamo huo utatolewa makao makuu ya chama mbele ya wafuasi wake waliosafiri kutoka kona mbalimbali za nchi.
Huku kukiwa na ulinzi mkali ulioimarishwa kuanzia askari wenye silaha za moto mpaka makachero waliovalia kiraia, eneo la mahakama lilifurika umati wa wafuasi wa chama cha Chadema, huku baadhi yao wakiwa wamevalia sare za chama chao zikiwa na ujumbe wa aina mbalimbali.
Nje ya ukumbi wa mahakama Mbowe alisindikizwa kuelekea kwenye karandinga na magereza kwa shangwe na nyimbo za wafuasi wake walionekana kutovunjika moyo juu ya yale yanayoendelea.
Lakini baadhi ya kina mama walionekana kumwaga machozi, huku wengine wakielezea hisia zao kutokana na uamuzi huo wa mahakama.
Kesi ya Mbowe aliyekamatwa kwa mara ya kwanza mkoani Mwanza wakati akiwa katika moja ya mikutano ya vuguvugu la kudai katiba mpya, imekuwa ikivuta hisia za wengi ndani nan je na hii leo kundi la wanadiplomasia wa nchi za Magharibi walifika mahakamani hapo kama sehemu ya mashuhuda.
George Njogopa, DW Dar es Salaam