1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwanasiasa Lema arejea Tanzania kutoka uhamishoni

1 Machi 2023

Mwanasiasa mashuhuri wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania Chadema Godbless Lema amerejea nchini Tanzania akitokea nchini Canada alipokuwa uhamishoni kwa kipindi cha miaka miwili.

https://p.dw.com/p/4O7Ys
Tansania Arusha | Oppositionspolitiker Godbless Lema aus kanadischem Exil zurückgekehrt
Picha: Kelvin Emmanuel

Lema aliondoka nchini humo yeye na familia yake enzi za utawala wa hayati Rais Dr. John Pombe Magufuli  kwa kile kilichoelezwa kwamba alihofia usalama wa Maisha yake.

Aliwahi kuwa mbunge wa jimbo la uchaguzi la Arusha mjini kwa tiketi ya chama chake cha Chadema na katika uchaguzi mkuu uliopita kwa mwaka 2020, mpinzani wake mkubwa Mrisho Gambo wa chama tawala  CCM aliibuka mshindi kulingana na matokeo yaliyotangazwa na tume ya taifa ya uchaguzi nchini humo. Anarejea nchini akiwa ni mwenyekiti wa Chadema kwa mikoa ya kanda ya kaskazini na mjumbe wa kamati kuu ya chama hicho. Amepokelewa na maelfu ya wafuasi wake na wanachama wa Chadema na baadaye akahutubia katika mkutano wa hadhara katika viwanja vya relini jijini Arusha.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aliyeingia madarakani kwa katiba  ya nchi hiyo baada ya kifo cha mtangulizi wake, hivi karibuni aliondoa zuio la mikutano ya hadhara kwa wanasiasa wa vyama vya upinzani, lililowekwa mwaka 2016 na utawala uliopita. Hali hiyo imefungua njia ya kufanyika kwa mikutano hiyo  ya hadhara na kuacha maoni mseto endapo mabadiliko haya ya Rais Samia ni ya kudumu?

Huyu ni mwanasiasa wa pili kurejea nchini hivi karibuni baada ya Makamu mwenyekiti wa Chadema na aliyekuwa mgombea uras wa Tanzania kupitia chama hicho katika uchaguzi mkuu uliopita Tundu Lisu kurejea nchini Januari 24 mwaka huu akitokea nchi Ubelgiji.

Veronica Natalis, DW Arusha