Mwanajeshi mmoja wa Israel auawa Ukingo wa Magharibi
27 Juni 2024Taarifa iliyotolewa na jeshi imeeleza kuwa mwanajeshi huyo ameuawa wakati wa operesheni kwenye eneo la Jenin. Vyombo vya habari vya Palestina vimeripoti kuwa wanajeshi wa Israel walivamia duka la dawa karibu na hospitali ya serikali ya Jenin, nje kidogo ya kambi ya wakimbizi ya Jenin na kuwakamata watu waliokuwemo ndani, na kuwapeleka kusikojulikana.
Mkaazi mmoja wa eneo hilo amesema tingatinga za Israeli ziliharibu miundombinu ndani ya kambi na katika mji wa Jenin. Chama cha wafungwa wa Kipalestina kimesema wanajeshi wa Israel waliwakamata watu 28, tisa kati yao wakiwa kutoka Jenin. Jeshi la Israel halijathibitisha kuhusu kukamatwa watu hao au kutoa taarifa zaidi kuhusu uvamizi huo.
Hayo yanajiri wakati ambapo Waziri wa Ulinzi wa Israel, Yoav Gallant amesema kuwa nchi yake haitaki vita na Lebanon, lakini wamejiandaa kwa lolote lile, ikiwa diplomasia itashindwa.
Akizungumza Jumatano na waandishi habari mjini Washington, Gallant amesema Israel haitaki kupigana vita kwa sababu sio jambo zuri kwa Israel, na kwamba wao wanapigana na wale tu wanaotaka kuwadhuru.
Israel kupambana na wanaotaka kuwadhuru
''Lakini ifahamike wazi kwamba vita vyetu sio na watu wa Gaza. Vita vyetu sio na watu wa Lebanon. Vita vyetu ni dhidi ya Hamas, Hezbollah, na utawala wa Iran ambao unawaunga mkono. Tumejitolea, na mimi binafsi nimejitolea kuwezesha kupelekwa misaada muhimu ya kiutu huko Gaza. Tunapigana tu na wale wanaotaka kutudhuru,'' alisisitiza Gallant.
Gallant amebainisha kuwa Hezbollah wanafahamu vizuri kwamba Israel inaweza kusababisha hasara kubwa nchini Lebanon iwapo vita vitaanzishwa. Waziri huyo wa ulinzi wa Israel amesema kuwa zaidi ya magaidi 400 wa Hezbollah wameuawa katika miezi ya hivi karibuni. Kwa mujibu wa takwimu za shirika la habari la AFP, takribani watu 481 wamekufa nchini Lebanon kutokana na mapigano kati ya Israel na Hezbollah tangu Oktoba 7, wakiwemo raia 94.
Wakati huo huo, jeshi la Israel leo limechapisha picha ambazo limesema zinamuonyesha mfanyakakazi wa shirika la Madaktari wasio na Mipaka akiwa amevalia sare za kijeshi zinazotumika vitani, katika mkutano na wanamgambo wa Gaza. Kulingana na jeshi hilo, Fadi al-Wadiya, ambaye aliuawa katika shambulizi la anga mapema wiki hii, alikuwa mtendaji muhimu wa kundi la Islamic Jihadi, na alihusika katika mpango wake wa roketi.
Watu wawili katika shambulizi la Israel huko Syria
Ama kwa upande mwingine, watu wawili wameuawa katika shambulizi la anga la Israel kusini mwa Syria. Shirika la habari la SANA limesema kuwa shambulizi hilo lililotokea usiku wa Jumatano katika milima ya Golan, limemjeruhi pia mwanajeshi mmoja.
Katika hatua nyingine, Ujerumani imewashauri raia wake kuondoka Lebanon, kutokana na hali ya wasiwasi kwenye mpaka wake na Israel. Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani imesema iwapo mzozo huo utakuwa mkubwa, usafiri wa anga unaweza ukatatizwa, hali itakayosababisha watu kushindwa kuondoka Lebanon kwa usafiri wa ndege.
(AFP, DPA, AP, Reuters)