Mwanablogu maarufu wa Uganda Fred Lumbuye akamatwa
5 Agosti 2021Mamlaka za Uganda leo zimethibitisha kukamatwa kwa mwanablogu maarufu Fred Lumbuye anayeishi uhamishoni nchini Uturuki. Hata hivyo bado haijafahamika ni vipi mwanablogu huyo anayeegemea upande wa upinzani na mkosoaji mkubwa wa utawala wa rais Yoweri Museveni ametiwa nguvuni.
Hadi sasa hakuna taarifa kamili zinazoeleza jinsi alivyokamatwa mwanablogu Fred Lumbuye kwenye ubalozi wa Uganda mjini Istanbul Uturuki. Ila kwa kauli ya waziri wa nchi wa masuala ya kigeni Henry Okello Oryem anayeshangaa kwa nini Waganda hawasherehekei kukamatwa kwake inaleta dhana kuwa palipo na moshi pana moto. Akihojiwa na DW kuhusu suala hilo waziri Oeyem amesema "Nilidhani kila mmoja wenu angekuwa akisherehekea kukamatwa kwa Lumbuye ambaye sasa atafikishwa mbele ya sheria lakini nyinyi mnaonekana kumhurumia tu:"
Soma zaidi: Naibu wa Rais Kenya Ruto azuiwa kwenda Uganda
Aidha maelezo ya msemaji wa idara ya upelelezi kwamba walikuwa wamewasilisha ombi kwa polisi wa kimataifa Interpol wakiwataka wamkamate Fred Lumbuye kwa kile kinachodaiwa kuwa hatia ya matumizi mabaya ya majukwaa ya kijamii na TEHAMA. Charles Twiine ndiye msemaji wa idara hiyo ya upelelezi, "Tulikwisha kumfungulia mashtaka manne na akirudishwa tutamfikisha mahakamani mara moja."
Kulingana na sheria za polisi wa kimataifa, wao huhusika katika kumkamata mshukiwa baada ya serikali ya nchi hiyo kutuma ombi kupitia mahakama ya taifa. Hadi sasa hakuna taarifa kwamba kuna agizo la mahakama ya Uganda Fred Lumbuye akamatwe.
Lumbuye amekamatwa kwa kile kinachodaiwa kuwa ya matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii
Ni kwa msingi huu ndipo chama cha NUP ambacho kinaelezea kuwa Fred Lumbuye ni mfuasi wao maarufu kinahoji kama serikali ya Uturuki itakuwa imezingatia sheria za kimataifa kuhusu kukamata raia wa nchi fulani nchini mwao.
Joel Senyonyi ni msemaji wa chama hicho kinachongozwa na Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, "Tunajaribu kufuatilia ukweli wa taarifa hizi kwa undani lakini inaonekana imethibitishwa amekamatwa, na tunachosikia wanataka kumrudisha Uganda. Lakini tunajaribu kuchunguza kama kuna mkataba wa aina hiyo kati ya Uturuki na Uganda."
Naye mwanaharakati wa haki za binadamu na pia mwanasheria Gawaya Tegule amesema, "Chini ya sheria za kimataifa taifa ambalo linalomba linatakiwa kutoa nyaraka za kuridhisha kuwa mtuhumiwa ana hatia ambayo si ya kisiasa basi lazima taifa husika kama Uturuki kumfikisha mahakamani kufikia maamuzi hayo.Changamoto ambayo naona ni kwamba Uturuki si nchi inayojulikana kuziheshimu haki za binadamu."
Mwanabloga Lumbuye ambaye pia ni mwanahabari amejijengea umaarufu kwenye mitandao ya kijamii kwa kutoa matamshi na taarifa zinazoshtumu serikali ya Uganda pamoja na watu binafsi mashuhuri ikiwemo mfalme wa Buganda.