Mwanaanga wa Ujerumani apaa anga za juu
6 Juni 2018Ni muungurumo wa roketi aina ya Soyuz lilipofyatuka kutoka mtambo wa kurushia maroketi yanayokwenda anga za mbali ulioko eneo la Baikonur nchini Kazakhstan. Wanasayansi watatu wanaosafiri katika roketi hilo wanakwenda katika ujumbe wa kitafiti uliopewa jina la ''Horizons'' ambao utadumu kwa miezi sita, ukifanyika umbali wa kilomita 400 kutoka anga la dunia.
Wanasayansi hao ni pamoja na Alexander Gerst wa Ujerumani ambaye ni mtaalamu wa masuala jiofizikia na maumbile ya volkano, Serena Aunon Chancellor, daktari wa Kimarekani aliyewahi pia kuwa rubani wa ndege za kivita, na Sergei Prokopyev, rubani wa ndege za kivita za Urusi.
Chombo wanachosafiri nacho, Roketi la Soyuz chapa MS-09 tayari kimeingia katika mzingo wa anga ya dunia, wakitarajiwa kutua kwenye kituo cha kimataifa cha anga za mbali, ISS Ijumaa wiki hii. Katika kituo hicho wataungana na wanaanga wengine watatu, Wamarekani wawili Drew Feustel na Ricky Arnold ambao wanatoka Shirika la Anga la nchi hiyo, NASA, pamoja na Oleg Artemyev wa shirika la anga la Urusi, Roscosmos.
Utafiti wa kimaabara nje ya mazingira ya dunia
Utafiti wa wanaanga hao unahusisha majaribio ya kimaabara yapatayo 250, kuhusu biolojia, sayansi ya dunia, utafiti wa kibinadamu, sayansi ya fizikia pamoja na ya kiteknolojia. Mkuu wa shirika la anga la Urusi Dmitry Rogozin na Balozi wa Marekani nchini Urusi Jon Huntsman ni miongoni mwa maafisa walioshuhudia kurushwa kwa roketi linalowabeba wanasayansi hao.
Hii ni mara ya pili kwa Alexander Gerst wa Ujerumani mwenye umri wa miaka 42 kusafiri kwenda anga za mbali. Mwaka 2014 alikuwa sehemu ya ujumbe mwingine uliojulikana kama Blue Dot. Lakini tofauti na ujumbe huo wa kwanza ambapo majukumu yake yalikuwa tu ya kiufundi, mara hii atakuwa kamanda wa ujumbe huu kwa muda wa miezi miwili. Familia yake imemtakia kila la heri katika safari yake kwenda anga za mbali, ikisema inaona fahari kwamba anashiriki kwa mara ya pili.
Mfano murua wa ushirikiano wa kimataifa
Mshauri mkuu wa Shirika la Anga la Ulaya ESA, Mark McCaughrean amesifu ushirikiano wa kimataifa kuhusu chombo cha anga za juu ISS, akisema ni mfano murua wa namna nchi za dunia zinazoweza kufanya kazi pamoja kwa masilahi ya utu. Chombo hicho hakitumiwi tu na Urusi, Marekani na Ulaya, bali pia Japan na China hukitumia katika shughuli zao za anga za juu.
Kabla ya kuruka kutoka kituo cha Baikonur, roketi la Soyuz limepata baraka za kasisi wa kanisa la Orthodox la Urusi kama ilivyo ada kwa shughuli kama hizo. Kama kawaida pia wanaanga watatu waliosafiri nalo wametia saini kwenye milango ya hoteli ya wanasayansi walikokuwa wakipiga kambi.
Mwandishi: Daniel Gakuba/dpae,ape
Mhariri:Josephat Charo