Marekani na Urusi zafarakana kuhusiana na Syria
5 Oktoba 2016"Wakuu wa taasisi zinazohusika na masuala ya usalama na siasa ya nje wanakutana kuzungumzia hatua "za kidiplomasia,kijeshi,kijasusi na kiuchumi" kabla ya kukutana na rais Barack Obama na kumkabidhi hatua hizo-wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani imesema huku ikishadidia umuhimu wa kupatikana ufumbuzi wa kisiasa.
Nchini Syria kwenyewe,wanamgambo wanaoelemea upande wa serikali wanaendelea kusonga mbele katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi ya mji wa kaskazini-Aleppo."Wanaelekea katika eneo la kati la mji huo" amesema hayo mkurugenzi wa shirika linalosimamia masuala ya haki za binaadam nchini Syria,Rami Abdel Rahmane. Lengo lao ni kuiteka mitaa ya karibu na mpaka wa magharibi ya Aleppo ili kuwazingira waasi kusini mashariki ya Aleppo.
Hujuma dhidi ya Aleppo zilizozoanza septemba 22 na vikosi vya serikali vikisaidiwa na Urusi ndio sababu iliyotajwa na Marekani inayounga mkono makundi ya upinzani,ili kuhalalisha uamuzi wa kusistisha mazungumzo pamoja na Urusi kuhusu Syria.
Moscow imetuma mtambo ziada wa makombora ya kinga ya angani
Moscow imesema imesikitishwa na uamuzi huo hata hivyo imeelezea matumaini yake kuona "busara ya kisiasa" inatawala mjini Washington."Uamuzi wa Marekani haumaanishi kwamba Urusi itaachana na mipango yake ya kusaidia jeshi la wanaanga la Syria katika kupambana na magaidi" msemaji wa ikulu ya Urusi-Kremlin Dmitri Peskov amesema.
Wakati huo huo wizara ya ulinzi ya Urusi imetangaza kutuma mtambo wa makombora ya kinga ya angani chapa S-300 katika mji wa mwambao wa Tartus,kaskazini magharibi ya Syria.
Kwa kupelekwa mfumo huo wa kinga ya makombora S-300,yakichanganyika na yale ya kimambo leo ya S-400 yaliyopelekwa Novemba mwaka jana,Urusi itakuwa inadhamini anga ya Syria kutoka vituo viwili muhimu- mji wa bandari waTartus na ule wa Hmeimim katika mkoa wa Lattakia .
Dazeni wauliwa karibu na mpoaka wa Uturuki
Wakati huo huo shirika linalosimamia masuala ya haki za binaadam linasema shambulio la angani dhidi ya kijiji cha wakurd kinachodhibitiwa na wanamgambo wa dola la kiislam IS karibu na mpaka wa kaskazini mwa Syria limepelekea watu kadhaa kuuwawa na dazeni kujeruhiwa . Itafaa kusema hapa kwamba katika eneo hilo,jeshi la Uturuki sawa na muungano wa kimataifa unaoongozwa na Marekani wanaendeleza mashambulio dhidi ya wanamgambo wa dola la kiislam.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/Reuiters
Mhariri: Grace Patricia Kabogo