1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaKosovo

Mvutano kati ya Kosovo na Serbia wazidi kufukuta

16 Juni 2023

Mvutano kati ya Kosovo na Serbia unaendelea kufukuta huku Kosovo ikisema itaimarisha usalama katika mpaka wake na jirani yake Serbia.

https://p.dw.com/p/4SgvI
Polisi wa Kosovo waliokamatwa na Serbia
Picha iliyotolewa na Serbia ikiwaonesha polisi wa Kosovo iliyowakamata. Kosovo inasema polisi hao walikamatwa ndani ya ardhi yake lakini Serbia inapinga hilo ikisema iliwakamata kwenye ardhi yake wakiwa na bunduki.Picha: Serbian Ministry of Interior via AP/picture alliance

Kosovo na Serbia ni majirani walioko kwenye mvutano unaozidi kuongeza wasiwasi hivi sasa katika Jumuiya ya Kimataifa, huku maafisa watatu wa polisi wa Kosovo wakishikiliwa na Serbia. Umoja wa Ulaya leo umetoa mwito wa kufanyika mkutano wiki ijayo mjini Brussels na viongozi hao wa Kosovo na Serbia, kujaribu kutafuta namna ya kuumaliza mvutano unaoongezeka katika eneo hilo.

Siku ya Alhamisi, Marekani ilitowa tamko ikizitaka pande zote mbili ziachane na mvutano unaosababisha machafuko. Kupitia  msemaji wake wa wizara ya mambo ya nje  Matthew Miller, Marekani ilisisitiza pia juu ya nchi hizo  kuzingatia  mpango wa Umoja wa Ulaya.

"Matarajio yetu kwa pande zote, ni kwamba tunaamini Kosovo na Serbia zinapaswa zote kuchukua hatua za mara moja kuachana na mivutano.Na hilo linajumuisha hatua ya kuachiwa huru bila masharti maafisa watatu wa polisi wa Kosovo waliokamatwa hivi karibuni. Tunaamini pande zote zinapaswa kufuata bila kuchelewa, mpango wa vipengele vitatu uliowekwa na Umoja wa Ulaya.'' amesema Miller.

Uingereza yajitosa kutoa rai ya kupunguzwa mvutano

Uingereza nayo pia kupitia wizara ya mambo ya nje imetowa tamko kama hilo la Marekani la kutaka pande zote mbili zisitishe mivutano.

Mvutano kati ya majirani hawa wawili umeongezeka baada ya kutokea machafuko mabaya katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita ambayo yaliongeza khofu juu ya kutokea tena kwa vita kama vilivyoshuhudiwa mnamo mwaka 1998 hadi 1999 ndani ya Kosovo yaliyosababisha zaidi ya watu 10,000 kuuwawa wengi wakiwa ni Wakosovo wenye asili ya kialbania.

Waziri Mkuu wa Kosovo Albin Kurti
Waziri Mkuu wa Kosovo Albin KurtiPicha: Erkin Keci/AA/picture alliance

Waziri mkuu wa Kosovo Albin Kurti siku ya Jumatano aliita hatua ya kukamatwa maasakari wake watatu kuwa utekaji nyara uliofanywa ndani ya Kosovo.

Kutokana na kisa hicho ametangaza kuimarisha usalama kwenye mpaka wake huku akiukosoa ujumbe wa kulinda amani wa Kimataifa, unaojulikana kama KFOR, unaoongozwa na jeshi la Jumuiya ya kujihami ya NATO,akisema umeshindwa kuchukuwa msimamo katika tukio hilo.

Kimsingi ujumbe huo una jukumu la kusimamia mipaka ya Kosovo upande wa Kaskazini. Waziri mkuu Kurt akizungumza na waandishi habari amewaonesha ramani ya eneo kilikotokea kisa hicho cha kukamatwa askari wake watatu,akisema kwamba polisi wa kikosi maaalum cha Serbia na kitengo cha jeshi waliingia kwenye ardhi ya Kosovo.

Serbia yapinga madai ya Kosovo kuhusu kukamatwa kwa polisi wake

Kosovo | Italienische KFOR Soldaten nach der FEstnahme von 3 Polizisten des Kosovo durch serbische Kräfte
Mvutano kati ya Serbia na Kosovo umekuwepo kwa miaka mingi na umezidi makali wiki za karibuni.Picha: Valdrin Xhemaj/REUTERS

Hata hivyo rais wa Serbia Aleksandar Vucic amesisitiza msimamo wa nchi yake kwamba polisi hao Wakosovo walikamatwa wakiwa ndani ya ardhi ya Serbia na waliulizwa walikuwa wakifanya kitu gani katika eneo hilo wakiwa na bunduki.

Kwa upande wa Ujumbe wa kulinnda amani wa KFOR, taarifa yao ya jana usiku ilisema wamewasiliana na wawakilishi wa pande zote mbili Kosovo na Serbia, kwa sababu, ujumbe huo haukuwepo katika eneo hilo wakati Polisi wa Kosovo walipokamatwa na maaskari wa Serbia.

Wiki iliypita waziri mkuu wa kosovo alilalamika juu ya kuwepo Upendeleo dhidi ya nchi yake kutoka Marekani na Umoja wa Ulaya, akisema pande hizo zinavumilia  kile alichokiita utawala wa kimabavu wa Serbia.

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW