Mvua kubwa na mafuriko yasababisha maafa nchini Ujerumani
15 Julai 2021Majimbo ya Rhineland-Palatinate na North Rhine-Westphalia (NRW) ndio yalioathirika zaidi nchini Ujerumani huku mafuriko hayo yakisababisha mito kuvunja kingo zake na kutishia kuporomosha nyumba zaidi. Msemaji mmoja wa polisi ameliambia shirika la habari la Ufaransa kwamba miili 18 ilipatikana katika eneo karibu na mji wa Magharibi wa Ahrweiler pekee. Mapema maafisa katika eneo hilo waliripoti kupotea kwa watu wapatao 70. Katika mji wa Euskirchen jimboni NRW, watu 15 wameripotiwa kufariki. Wakazi waliokata tamaa walitafuta hifadhi juu ya paa za nyumba zao huku helikopta zikizunguka juu kuwaokoa kutoka kwa maji yaliyokuwa yakiongezeka.
Waziri Mkuu wa jimbo la NRW Armin Laschet anayewania kumrithi Angela Merkel kama kansela wa Ujerumani, alikatisha mkutano wa chama chake katika jimbo la Bavaria kukagua uharibifu katika jimbo lake lenye idadi kubwa ya watu. Laschet amesema kuwa kwasasa wanahitaji msaada lakini hawawezi kubainisha kiasi cha msaada huo kwasababu hawajafahamu kiasi cha hasara iliopatikana . Hata hivyo amesema kuwa jimbo la North Rhine Westphalia linasimama pamoja kwa mshikamano katika hali hilo.
Maafa katika mataifa jirani
Nchini Ubelgiji, mto Vesdre ulivunja kingo zake na kusababisha kufurika kwa maji yalioenea katika barabara za Pepinster karibu na mji wa Liege huku yakisababisha kuporoka kwa majumba kadhaa. Meya wa eneo hilo Philippe Godin amelithibitishia shirika la habari la RTBF kwamba nyumba kadhaa zimeporomoka. Haijabainika iwapo wakazi wote walinusurika bila majeraha.
Vyombo vya habari nchini Uholanzi vimeripoti kuwa mamlaka katika mji wa Kusini wa nchi hiyo Valkenburg ulioko karibu na mpaka kati ya Ujerumani na Ubelgiji, iliwaondoa wazee waliokuwa katika nyumba ya wazee usiku kucha huku mafuriko hayo yakigeuza barabara kuu ya mji huo wa kitalii kuwa mto. Serikali ya Uholanzi imetuma takriban wanajeshi 70 katika jimbo la Kusini la Limburg Jumatano jioni kusaidia katika shughuli ya uokoaji.
Rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen ameomba kutolewa kwa msaada kwa wale walioathirika. Katika ujumbe kupitia mtandao wake wa twitter, Von der Leyen ameandika kwamba mawazo yake yako pamoja na familia za waathiriwa wa mafuriko nchini Ubelgiji, Ujerumani, Luxembourg na Uholanzi pamoja na wale waliopoteza makazi yao na kuongeza kuwa Umoja wa Ulaya uko tayari kusaidia.