Muziki wa Rumba watangazwa kuwa sehemu ya turadhi za UNESCO
15 Desemba 2021Mtindo huu wa muziki una asili yake katika ufalme wa kale wa Kongo uliokuwa kwenye fukwe za magharibi ya Afrika ya Kati. Takriban miaka 500 iliyopita, ngoma iitwayo Nkumba ilichezwa huko, ikigonganisha kitovu na kitovu kingine kwa mtindo unaojulikana leo kama "Collé-Sérré".
Uamuzi wa kuuinua muziki wa Rumba ulitangazwa na UNESCO hapo jana, baada ya kuchunguza baadhi ya maombi sitini ya muziki, yakiwemo ya Rumba yaliyowasilishwa kwa pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na nchi jirani ya Congo-Brazzaville.
Kupitia tovuti yake, shirika la umoja wa mataifa la elimu, sayansi na utamaduni (UNESCO) limeshuhudia kwamba Rumba inachukuliwa kuwa sehemu muhimu na wakilishi ya utambulisho wa watu wa Congo, waonaishi kwenye ardhi ya Congo na pia ugenini. Pia inaruhusu kukuza maadili ya kijamii na kitamaduni ya eneo hilo, pamoja na mshikamano wa kijamii, wa vizazi na wa umoja.
Katika hali yake ya kisasa, rumba ya Congo imenakili mtindo kwa rumba ya Cuba iliovuma katika miaka ya 1930 na 1940. Tangu wakati huo, rumba imeendelea kubadilika, ikivumishwa na wasanii wengi, kuanzia na Tabu Ley Rochereau, Papa Wemba, au Grand Kallé. Kinshasa na Brazzaville zinahisi kwamba kutambuliwa huko na UNESCO kutaipa rumba sifa mpya.