1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vyama vya mrengo wa kushoto vyashinda uchaguzi Ufaransa

8 Julai 2024

Muungano wa vyama vya mrengo wa kushoto wa New Popular Front, NFP umepata ushindi dhidi ya chama cha mrengo wa kulia cha National Rally (RN) katika duru ya pili ya uchaguzi wa bunge nchini Ufaransa.

https://p.dw.com/p/4i0mq
Uchaguzi wa bunge | Paris
Muungano wa vyama vya mrengo wa kushoto washinda duru ya pili ya uchaguzi UfaransaPicha: Lionel Urman/ABACAPRESS/IMAGO

Muungano huo wa mrengo wa kushoto umejishindia viti 182, muungano wa siasa za wastani wa rais Macron ukipata viti 168 huku chama cha National Rally (RN) na washirika wake wamejikusanyia viti 143.

Hata hivyo hakuna muungano ulioweza kupata wingi wa viti bungeni, jambo linalotishia kuitumbukiza Ufaransa katika msukosuko wa kisiasa na kiuchumi.

Wafaransa wapiga kura duru ya pili ya uchaguzi wa Bunge

Muungano wa NFP umesema utatangaza jina la mgombea wa nafasi ya Waziri Mkuu.

"Kwa kuzingatia mantiki ya kitaasisi, ni juu yetu sasa kutafuta suluhu. Waziri Mkuu mzuri ni lazima aitulize nchi, na alete mshikamano ndani ya kundi lake," alisema Marine Tondelier Kiongozi wa chama cha kijani EELV kilicho sehemu ya muungano huo Marine Tondelier.

Waziri Mkuu wa nchi hiyo Gabriel Attal, anayepanga kujiuzulu, amesema nchi yake inakabiliwa na hali ya kisiasa ambayo haijawahi kushuhudiwa.