Munich: Mkutano juu ya usalama kufanyika kwa siku tatu
15 Februari 2019Waziri von der Leyen aliufungua mkutano huo pamoja na waziri mwenzake wa ulinzi wa Uingereza Gavin Williamson. Von der Leyen amesema ukweli ni kwamba magaidi wa dola la Kiislamu wamebadilisha mkakati wao na kwamba sasa wanaendesha opereshani zao kichini chini na wanajenga mitandao ambayo ni sehemu ya muundo wa dunia nzima.
Mkutano huo wa 55 wa masuala ya usalama umeanza hii leo mjini Munich kusini mwa Ujerumani na unazingatiwa kuwa jukwaa kubwa kabisa la kimataifa linalowaleta pamoja, wanasiasa, wataalamu wa masuala ya usalama na ulinzi pamoja na wadau wa masuala ya haki za binadamu
Kwenye mkutano huo wa siku tatu wakuu wa nchi na viongozi wa serikali wapatao 40 watajadili mustakabal wa Ulaya, uhusiano baina ya Marekani na nchi za Ulaya na pia watazungumzia juu ya mkataba wa kudhibiti makombora ya nyuklia ya masafa ya kati. Wajumbe kwenye mkutano huo pia watazungumzia juu ya uhusiano baina ya Urusi na nchi za magharibi, hali ya Mashariki ya Kati,mgogoro wa nchini Venezuela na dhima ya China katika masuala ya dunia.
Kaimu waziri wa ulinzi wa Marekani Partick Shanahan amesema Marekani itaunga mkono harakati za kupambana na magaidi wanaojiita dola la kiislamu katika maeneo mengine nje ya Iraq na Syria. Akihutuba kwenye mkutano wa mjini Munich Shanahan alizitaja nchi hizo kuwa pamoja na Afghanistan,Ufilipino na eneo la Sahel ambako magaidi hao wanaendelea kujikita. Waziri huyo amesema hata ikiwa Marekani inayaondoa majeshi yake kutoka Syria, itaendelea kuwaunga mkono washirika wa eneo hilo katika mapambano yao dhidi ya magaidi wa dola la kiislamu.
Makamu waziri wa ulinzi wa Marekani Shanahan kwa mara nyingine alilaumu Ujerumani na kusema kuwa mchango wa nchi hiyo hautoshi. Ayalisema hayo kwenye mkutano na mawaziri wenzake wa nchi za NATO uliofanyika mjini Brussels.
Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg amesema siku atazungumza na waziri wa Mambo ya nje wa Urusi Sergey Lavrov juu ya ukiukwaji wa mkataba wa silaha za nyuklia, Stoltenberg amesema mazungumzo ni muhimu wakati mvutano ukiwa umepamba moto.
Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Ursula von dea Leyen amesema jumuiya ya kijeshi ya NATO itaendelea kuwa mfungamano wa kijeshi na kisiasa utakaokuwa chaguo la kwanza kwa usalama wa Ujerumani. Waziri huyo ametaka kuwepo na usawa zaidi ndani ya mfungamano huo na amekiri kwamba wito wa Marekani juu ya kuleta haki katika kubeba majukumu ni wa halali kabisa.
Mwenyekiti wa mkutano balozi Wolfgang Ischinger pia amefahamisha kwamba juhudi za kuleta maridhiano juu ya Ukraine zinaweza kufanyika kandoni ya mkutano baina ya Urusi na Ukraine lakini amesema Ufaransa na Ujerumani pia zinaweza kushiriki.
Waandalizi wa mkutano wanatarajia mahudhurio makubwa. Kulingana na taarifa, wanaisasa 600, wataalamu, wafanyabiashara na watetezi wa haki za binadamu wanatazamiwa kushiriki kwenye mkutano huo. Mawaziri wa mambo ya nje 50 na wenzao wa ulinzi 30 pia wanatarijiwa kuwapo kwenye mkutano wa mjini Munich.
Mwandishi:Zainab Aziz/DPA/AP
Mhariri: Josephat Charo