1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mugabe na Tsvangirai-Majadiliano ya kugawana Madaraka

P.Martin11 Agosti 2008

Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe na kiongozi wa upinzani Morgan Tsvangirai leo wanatazamiwa kuendelea na majadiliano yao baada ya hiyo jana kutofanikiwa kutia saini makubaliano ya kugawana madaraka.

https://p.dw.com/p/EuiV
South African President Thabo Mbeki, left, is accompanied by Zimbabwean President Robert Mugabe, center, on Mbeki's arrival for talks in Harare Saturday, Aug. 9. 2008. Mbeki came to the country to mediate talks between Mugabe's party and the opposition. (AP Photo)
Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe(kulia) akimpokea Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini alipowasili Harare Agosti 9,2008.Picha: AP

Majadiliano hayo kati ya Rais Mugabe wa chama cha ZANU-PF na kiongozi wa upinzani Morgan Tsvangirai wa Movement for Democratic Change-MDC-yanafanywa chini ya upatanishi wa Rais wa Afrika Kusini Thabo Mbeki katika mji mkuu wa Zimbabwe Harare.

Baada ya kuwa na majadiliano kwa takriban saa 14 katika hoteli ya Rainbow Towers,Mugabe mwenye miaka 84 alikuwa wa kwanza kutoka nje mapema asubuhi ya leo.Akawaambia maripota ambao hawakuruhusiwa kuhudhuria mkutano huo,kuwa majadiliano bado hayajamalizika.Alisema,kama ilivyo kawaida katika majadiliano ya aina hiyo,kuna masuala ya utata lakini hii leo wataondosha tofauti zilizopo.

Wakati huo huo kiongozi wa tawi lililojitenga na chama cha MDC,Arthur Mutambara anaeshiriki katika mazungumzo hayo,alisema majadiliano hayo ni kazi inayoendelea.Lakini Tsvangirai alikataa kueleza cho chote.

Rais Mbeki aliwasili Harare siku ya Jumamosi kuwahimiza viongozi wa ZANU-PF na wa matawi mawili ya MDC kukamilisha majadiliano yaliyoanza takriban majuma mawili yaliyopita nchini Afrika Kusini.Mugabe alieapishwa rais kwa miaka mitano ijayo hapo mwezi Juni,kufuatia uchaguzi uliolaaniwa na wengi kuwa uwongo tu,alikubali kwa shingo upande,kushiriki katika majadiliano hayo baada ya kushinikizwa na Umoja wa Afrika.Hata ile hali mbaya mno ya uchumi nchini Zimbabwe inayodhihirika kwa mfumko wa bei uliopindukia asilimia milioni 2 nukta mbili, imemlazimisha Mugabe kwenda katika meza ya majadiliano,kinyume na msimamo wake wa kawaida wa kubisha.

Serikali za nchi za magharibi zimeahidi kuisaidia Zimbabwe kujitoa kutoka janga hilo la uchumi,ikiwa chama cha MDC na Tsvangirai watakuwa na dhima kuu katika serikali ya umoja wa taifa.Ripoti zilizotolewa baada ya majadiliano ya Afrika Kusini,zimeashiria kuwa Tsvangirai atakuwa waziri mkuu katika serikali mpya.Miongoni mwa mada zinazochelewesha maafikiano kupatikana ni suala la kugawana madaraka kati ya Mugabe na Tsvangirai,muda wa serikali mpya kubakia madarakani na wizara za kugawana kati yao.

Ni matumaini ya Wazimbabwe kuwa kutapatikana suluhisho litakalowaokoa kutoka ukandamizaji wa kisiasa uliokuwa ukiongezeka tangu mwongo mmoja na pia shida za kiuchumi zinazowakabili kila siku,chini ya utawala wa Rais Mugabe.Mwezi wa Julai,Umoja wa Afrika ulitoa wito kwa Mugabe na Tsvangirai kugawana madaraka,baada ya Mugabe kugombea duru ya pili ya uchaguzi wa rais peke yake hapo Juni 27.Uchaguzi huo ulisusiwa na Tsvangirai baada ya baadhi ya wafuasi wake kuuawa na wanamgambo wanaomuunga mkono Mugabe,kufuatia ushindi wa Tsvangirai katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais uliofanywa Machi 29.