Mugabe aapishwa rasmi
22 Agosti 2013Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe ameapishwa kwa ajili ya muhula mwengine wa miaka mitano kuongoza nchi hiyo katika sherehe kubwa kwenye uwanja mkubwa mjini Harare, ambao unao uwezo wa kuwapokea watu 60,000.
Katika kiapo mbele ya Jaji Mkuu Godfrey Chidyausiku maelfu ya wafuasi wake, Mugabe ameahidi "kuilinda na kuitetea katiba ya Zimbabwe".
Wakuu wa nchi 40 walikuwa wamealikwa katika sherehe hizo, ambazo zimesusiwa na upinzani. Msemaji wa kiongozi wa upinzani nchini humo, Morgan Tsvangirai, amesema kiongozi huyo hawezi kushiriki katika kile alichokiita 'sherehe ya mwizi'.
Wakati wa kuapishwa kwake, pia itakuwa na nafasi ya rais huyo kutoa hotuba zake kali hususani za kuyashutumu mataifa ya Magharibi kutokana na vikwazo iliyoiwekea Zimbabwe.
Tofauti na sherehe zilizopita kumwapisha Mugabe ambazo hazikuwa na shamrashamra, hii ya mwaka huu imepewa umuhimu mkubwa.
Changamoto za Mugabe
Wachambuzi wanasema hali hiyo inadhamiria kujaribu kuhalalisha ushindi wa Robert Mugabe katika uchaguzi wa rais wa tarehe 31 Julai, ambao ulikumbwa na utata.
Huu ni muhula wa saba wa Robert Mugabe kama rais wa Zimbabwe na wachambuzi wanaonya kuwa amri ya mahakama hiyo kutupilia mbali madai ya Tsvangirai aliyepinga matokeo ya uchaguzi ni kichocheo cha ukandamizaji wa kisiasa.
Tsvangirai alimshitaki Mugabe kupinga matokeo ya uchaguzi uliofanyika mwishoni mwa Julai, ambapo Mugabe alitangazwa mshindi dhidi ya mpinzani wake huyo ambaye pia alikuwa waziri mkuu wa nchi hiyo kabla ya uchaguzi.
Tume ya Uchaguzi nchini Zimbabwe ilitangaza kuwa chama cha ZANU-PF kilishinda theluthi tatu ya idadi ya viti bungeni na kwamba Mugabe alipata ushindi wa zaidi ya asilimia 60 ya kura zilizopigwa.
Lakini wiki iliyopita Tsavangirai alifutilia mbali madai yake dhidi ya ZANU-PF, baada ya kuyapeleka katika Mahakama Kuu kupinga matokeo ya uchaguzi, akisema hana imani ya kupata haki mahakamani huko. Siku ya Jumanne mahakama hiyo ilisema uchaguzi huo ulikuwa huru na haki na kuwa ulizingatia matakwa ya raia wake
Tsvangirai anadai kuwa takribani wapiga kura milioni moja waliondolewa kwenye vituo vya kupigia kura katika maeneo ya mijini yanayoaminiwa kuwa ni ngome yake ya kisiasa, ingawa mahakama ilifutilia mbali madai hayo.
Hata hivyo, msemaji wa Tsvangirai, Douglas Mwonzora, ameiambia IPS kuwa hakushangazwa na uamuzi uliotolewa na mahakama hiyo, kwa kuwa walilijua suala hilo mapema.
Sherehe za kuapishwa kwa Rais Mugabe zilikuwa zimecheleweshwa kufanyika kutokana na kesi hiyo.
Jumuiya za Kiafrika zamuunga mkono Mugabe
Uchaguzi huo umeleta hisia tofauti ndani na nje ya Zimbabwe ingawa pia ulisifiwa na mashirika ya Kiafrika yaliyotuma waangalizi wake katika uchaguzi huo, na kutokana na hilo jamii ya kimataifa italazimika kuamua kuendelea kutomtambua Mugabe au kutafuta njia za kushirikiana naye ili kuleta demokrasia ya kweli nchini humo
Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) ilipongeza kuchaguliwa kwa Rais Mugabe, huku wananchi wake wakiwa katika wakati mgumu. SADC ilifika umbali wa kuyaomba mataifa wafadhili kuiondolea vikwazo Zimbabwe baada ya uchaguzi huu, kwani "uliakisi matakwa ya Wazimbabwe".
Lakini Umoja wa Ulaya, ambao umelegeza baadhi ya vikwazo vyake kwa Zimbabwe, unatafakari jambo hilo kwa kina baada ya kuwa na wasiwasi juu ya madai ya udanganyifu na kukosekana kwa uwazi katika uchaguzi huo.
Swali linaloulizwa kwa sasa ni iwapo rais huyo anaweza kweli kumaliza hatamu yake ya miaka mitano kutokana na umri wake mkubwa na iwapo atafariki au kuachia ngazi ni nani atakayemrithi. Afya ya rais huyo aliye na umri wa miaka 89 na aliyeongoza Zimbabwe kwa takriban miaka 33 inatiliwa shaka.
Awali kumekuwa na maswali mengi juu ya afya yake. Mugabe alikana kwamba anaugua saratani ya kibofu na kusema ana nia ya kuongoza kipindi chake chote cha miaka mitano.
Ukiacha suala hili linaloonekana kutoa changamoto kwa taifa hilo la kusini mwa Afrika ambalo ni tajiri kwa madini na linalokumbana na msukosuko wa kisiasa, kwa ujumla Mugabe anakabiliwa na vitisho vichache tu, kwani mpinzani wake wa muda mrefu Tsvangirai anaonekana sasa kumalizika.
Stephen Chan, Profesa wa maswala ya uhusiano wa kimataifa katika taasisi ya mafunzo ya Afrika anasema "Mugabe na Tsvangirai wamepambana vikali katika uchaguzi uliopita kwa njia moja au nyengine. Iwapo kumetokea wizi wa kura au la bado uchaguzi huo utabakia kuonekana kama zoezi la kihistoria lililoleta mabadiliko."
Mwandishi: Flora Nzema/IPS/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef