1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Muethiopia Tedros ndiye mkuu mpya wa WHO

24 Mei 2017

Tedros Adhanom amechaguliwa kuwa mkurugenzi mkuu wa shirika la afya duniani WHO na mtu wa kwanza kutoka Afrika kuwa mkuu wa Shirika hilo la kimataifa.

https://p.dw.com/p/2dV2w
Tedros Adhanom Ghebreyesus ehem. Außenminister Äthiopien
Tedros Adhanom akitoa hotuba yakePicha: DW/T. Woldeyes

Shirika hilo linadaiwa kuhitaji kufanyiwa mabadiliko makubwa. Waziri huyo wa zamani wa afya na  wa mambo ya nchi za nje wa Ethiopia aliyeapa kuleta mabadiliko, aliwashinda David Nabarro wa Uingereza na Sania Nishtar wa Pakistan baada ya awamu tatu za upigaji kura katika uchaguzi uliofanyika huko Geneva nchini Uswisi, Jumanne.

Wafuasi wa Tedros mwenye umri wa miaka 52 na ambaye pia ni mtaalamu wa ugonjwa wa malaria, walimzunguka baada ya matokeo kutangazwa katika ukumbi wa kupigia kura katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa, huku mmoja wa wafuasi hao akiwa amebeba bendera ya Ethiopia.

Alipata kura 133 huku Nabarro akijinyakulia kura 50 na mgombea wa tatu Sania Nishtar kutoka Pakistan akiwa alibanduliwa katika raundi ya kwanza ya kura.

Huduma ya afya kwa walio fukara duniani ndicho kipau mbele chake

Katika hotuba yake mkuu huyo mpya wa shirika hilo la afya duniani, aliahidi kuhakikisha anarejesha uaminifu wa WHO uliokuwepo kwa mataifa mataifa yote wanachama na kila mmoja duniani. Alisema utoaji wa huduma ya afya hususan kwa watu maskini zaidi duniani ndilo litakalokuwa jambo atakalolipa kipau mbele.

David Nabarro
David Nabarro aliyeshindwa na TedrosPicha: Imago/Xinhua

"Kamwe sitowasahau watu tunaowahudumia kwasababu yote tunayoyafanya ni kwa ajili yao, lakini hawako hapa Geneva wakisikiliza hotuba zetu ila wanaugua kutokana na magonjwa yanayoweza kuzuilika na umaskini," alisema Tedros, "Pamoja tutayaokoa maisha ya ndugu zetu walio fukara zaidi duniani, hili ndio ahadi yangu kwenu."

Tedros atakuwa mkurugenzi mkuu wa 8 wa shirika hilo la afya lililoanzishwa mwaka 1948 na wa kwanza kuchaguliwa katika kinyang'anyiro kikali cha uchaguzi mbele ya bunge. Wakuu wa zamani wa WHO walichaguliwa na bodi ya utendaji ya shirika hilo na idhini ya bunge kimsingi ilikuwa ni kama kuupigia muhuri uamuzi huo.

Ameshutumiwa kwa madai ya kuficha mkurupuko wa kipindupindu Ethiopia

Tedros alihudumu kama waziri wa afya wa Ethiopia kati ya mwaka 2005 na 2012 kisha akahudumu kama waziri wa mambo ya nje kwa miaka minne. Alisifiwa mno kwa kuongeza idadi ya wafanyakazi katika idara ya afya ya Ethiopia wakati wake kama waziri na kuiboresha sekta hiyo. Daktari Thomas Frieden aliyekuwa mkurugenzi wa zamani wa Kituo cha Marekani cha kudhibiti na kuzuia magonjwa, alisifu kuchaguliwa kwa Tedros akisema alifanikiwa nchini Ethiopia katika wadhfa kama huo.

Sania Nishtar
Sania Nishtar kutoka Pakistan alishindwa katika raundi ya kwanzaPicha: Imago/Xinhua

Lakini alishutumiwa pia kwa madai ya kuficha mkurupuko wa kipindupindu nchini Ethiopia na kulikuwa na maandamano ya karibu watu 200 hivi Jumanne nje ya makao makuu ya Umoja wa Mataifa.

Ataanza muhula wake wa miaka 5 baada ya Margaret Chan raia wa Hong Kong kukamilisha kipindi chake cha kuliongoza Shirika hilo la Afaya Duniani tarehe 30 mwezi ujao wa Juni.

Mwandishi: Jacob Safari/APE/AFPE/Reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman