Mtuhumiwa wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda akamatwa
16 Mei 2020Felicien Kabuga mwenye umri wa miaka 84 alikuwa mtuhumiwa aliyewekwa kwenye mstari wa mbele. Kitita cha dola milioni tano kilitengwa kwa yeyote ambaye angetoa habari za kuwezesha kukamatwa kwake. Kwa muda wote huo alikuwa anatumia majina bandia.
Wizara ya mambo ya ndani ya Ufaransa imesema polisi walimkamata leo alfajiri.Kwa mujibu wa taarifa ya mahakama ya Umoja wa Mataifa iIiyoanzishwa kwa ajili ya kuhumu kesi za uhalifu, IRMCT, Kabuga alihukumiwa mnamo mwaka mwaka 1997 kwa mokosa saba ya uhalifu ikiwa pamoja na ya mauaji ya halaiki, kuchochea mauaji na kushiriki katika mauaji.
Kabuga ambae ni Mhutu na mfanyabiashara anakabiliwa na mashtaka ya kuwafadhili wanamgambo waliowaua Watusi wapatao 800,000 na Wahutu waliokuwa na msimamo wa wastani katika muda wa siku 100 mnamo mwaka 1994. Tangu mwaka huo wa 1994 amekuwa anaishi bila ya kuchuliwa hatua katia nchi za Ujerumani,Ubelgiji, Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, Kenya na Uswisi licha ya kujulikana kuwa aliwalipa wanamgambo kufanya mauaji.
Kabuga atafikishwa kwenye mahakamani ya rufani ya mjini Paris na baadae atapelekwa kwenye mahakama ya kimataifa ya Mjini The Hague. Watuhumiwa wengine wawili wa mauaji ya halaiki ya Rwanda, Augustin Bizimana na Protais Mpiranya bado wanasakwa na vyombo vya sheria vya kimataifa.
Mara tu baada Kabuga kukamatwa, mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama ya Umoja wa Mataifa, Serge Brammertz amesema kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo ni ishara kwamba wote waliohusika na mauaji ya Rwanda watawajibishwa hata ikiwa imeshapita miaka 26 tangu kufanyika kwa uhalifu huo
na kwamba hatua hiyo inathibitisha dhamira ya mahakama ya Umoja wa Mataifa ya mjini Arusha,Tanzania kuwa wote waliohusika na mauaji hayo watafikishwa mahakamani. Kabuga anatarajiwa kujibu mashtaka kwenye mahakama ya hiyo ya Umoja wa Mataifa ya mjini Arusha.
Mwendesha mashtaka huyo ameeleza kuwa kadhia ya kushikwa mtuhumiwa huyo imetokana na ushirikiano kati ya idara za sheria za Ufaransa na za nchi nyingine ikiwa pamoja na Marekani, Rwanda, Ubelgiji, Uingereza na nchi nyingine kadhaa. Felicien Kabuga alihusika na manunuzi makubwa ya mapanga, majembe na vifaa vingine vya kilimo akiwa anajua vilikusudiwa kutumiwa kama silaha wakatia wa mauaji ya halaiki.
Vyanzo:RTRE/AFP/AP