Mti unapoanguka… - Kukatwa kwa misitu barani Afrika
13 Machi 2014Katikati ya bara la Afrika, utakuta msitu wa pili kwa ukubwa duniani unaoanzia Jamhuri ya Kidemkrasai ya Kongo hadi nchi jirani. Msitu huu pamoja na misitu mingine ya zamani barani Afrika ina umuhimu mkubwa kwa ajili ya bioanuai na tabianchi ya dunia nzima. Hata hivyo, Afrika ndilo bara linaloongoza duniani katika kupoteza misitu kwa wingi.
Katika baadhi ya maeneo, misitu imepotea kabisa kama vile kwenye nchi nyingi za Afrika Magharibi. Katika maeneo mengine, makampuni ya kimataifa ya kutengeneza mbao hukata miti iliyobakia kwa kasi kubwa. Mfumo wa kilimo wa kukata na kuchoma kwa ajili ya kilimo cha kujikimu pamoja na ukataji wa miti kwa ajili ya kutengeneza mkaa husababisha misitu zaidi kupotea.
Mchezo huu wa redio unalenga kuongeza ufahamu juu ya jukumu muhimu la misitu la kuratibu tabianchi na kuhifadhi maji. Masimulizi haya yanatokea katika eneo lenye mapigano ya wenyewe kwa wenyewe na yanaonyesha namna ambavyo ukataji wa miti umeharibu maisha ya vijijini na kuleta ugomvi kati ya jamii mbili za wakulima.
Watu hawa sasa wanalazimika kuishi pamoja katika kambi ya wakimbizi ya Dovani na wanaanza kutafuta suluhu za wakati wa baadaye na kufahamu njia mbadala na endelevu za kutumia misitu.
Vipindi vya Deutsche Welle vya Noa Bongo! Jenga Maisha Yako vinapatikana katika lugha sita: Kiingereza, Kiswahili, Kifaransa, Kihausa, Kireno na Kiamhara.