Kiongozi wa zamani Guinea ahukumiwa miaka 20 jela
1 Agosti 2024Camara amehukumiwa kwa kuhusika na makosa hayo dhidi ya ubinadamu kutokana na mauaji yaliyofanywa na wanajeshi chini ya utawala wake katika uwanja wa mpira mwaka 2009.
Kando ya kiongozi huyo wa zamani wa kijeshi, mahakama ya uhalifu ya Guinea imewahukumu pia maafisa wengine saba wa ngazi ya juu waliokuwa wakikabiliwa na tuhuma za mauaji, utekaji nyara na ubakaji zilizobadilishwa hadhi na kutambuliwa kama uhalifu dhidi ya ubinadamu. Wengine wanne katika shauri hilo waliachiliwa huru.
Katika kesi hiyo iliyoanza kusikilizwa Novemba 2022, zaidi ya watu 100 waliosalimika na ndugu wa waathiriwa walitoa ushahidi. Rais wa chama cha waathiriwa wa uhalifu huo Asmaou Diallo ni miongoni mwa waliupongeza uamuzi uliotolewa na mahakama Jumatano licha ya baadhi ya watu kusema kuwa adhabu ya Camara haitoshi.
Septemba 28 2009, maelfu ya waandamanaji walikusanyika katika uwanja wa mpira wakipinga mipango ya Moussa "Dadis" Camara kugombea kiti cha Urais. Wakati wakifanya hivyo, wanajeshi walianza kuwafyatulia risasi na kuwabaka wanawake.
Wengi wa waathiriwa wa mauaji hayo walipigwa risasi au kuchomwa visu wakati wanawake walitolewa kwa nguvu mafichoni na kufanyiwa ubakaji na makundi ya watu waliokuwa na sare za jeshi. Wengi wa waandamanaji walishindwa kukimbia baada ya baadhi ya wanajeshi kuuzunguka uwanja na kuweka vizuizi katika milango ya kutokea.
Tuhuma za mauaji na ubakaji zilikanushwa na jeshi
Utawala wa kijeshi wa wakati huo chini ya kiongozi huyo ulitoa maelezo kuwa, sehemu ya wanajeshi wake walioshindikana kudhibitiwa ndiyo waliofanya mauaji na vitendo vya ubakaji. Licha ya maelezo hayo, Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch katika ripoti yake lilibainisha kuwa wasaidizi wa ngazi ya juu wa Camara walikuwa uwanjani na hawakuchukua hatua yoyote kuzuia mauaji.
Akizungumza baada ya hukumu iliyotolewa Jumatano, wakili wa haki za kimataifa wa shirika hilo Tamara Aburamadan, amesema kuwa uamuzi huo unatuma ujumbe wa wazi kwa wanaohusika na uhalifu nchini Guinea na kwingineko duniani kuwa haki inaweza kupatikana.