Mtafaruku wa kisiasa Malaysia, Mahathir ajiuzulu
24 Februari 2020Hali hii imekuja baada ya miezi kadhaa ya kupanda kwa hali ya wasi wasi katika kile kinachofahmika kama " muungano wa matumaini", ambao uliingia madarakani kwa kushangaza mwaka 2018 dhidi ya serikali iliyokuwa imetumbukia katika rushwa ambayo iliiongoza Malaylasia kwa miongo sita.
Lakini kulikuwa na miito kwa Mahathir , kiongozi mkongwe kabisa duniani mwenye umri wa miaka 94, kuendelea kubakia madarakani kutoka kwa washirika ambao wanasisitiza kuwa hakuunga mkono kuundwa kwa serikali mpya na ameondoka kwa kukasirishwa na njama hizo.
Patashika hiyo ya kisiasa ilianza siku ya Jumapili wakati mahasimu wa Anwar walipowasili kutoka muungano unaotawala na upinzani walipofanya vikao kadhaa mjini Luala Lumpur, na kuzusha uvumi kuwa ushirika mpya unaundwa.
Muungano huo unaripotiwa kuwa ungemtenga Anwar, mrithi mteule wa Mahathir na kiongozi mkuu wa zamani wa upinzani ambaye alifungwa jela kutokana na madai yenye shaka ya kulawiti, na kuzuwia kuingia kwake madarakani kuwa waziri mkuu.
Wakati hatima ya serikali bado haifahamiki hadi leo Jumatatu, Mahathir aliwasilisha barua ya kujiuzulu kwa mfalme. Mfalme amekubali kujiuzulu kwa Mahathir, lakini amemteua kuwa kiongozi wa mpito hadi waziri mkuu mpya atakapopatikana, kwa mujibu wa taarifa rasmi.
Waziri mkuu atoa uhakika
Anwar, ambaye amekuwa na uhusiano usio mzuri na Mahathir, amesema waziri mkuu amemhakikishia , kwamba hakuhusika kabisa, na juhudi za kuunda serikali mpya, na alikuwa wazi kabisa kuwa hawezi kabisa kufanyakazi na wale ambao wanajihusisha na utawala wa zamani".
Muungano mpya unaopendekezwa unaripotiwa kuwa unajumuisha chama cha United Malays National Organisation, UMNO, cha kiongozi wa zamani Najib Razak, ambacho kiondolewa madarakani miaka miwili iliyopita.
Anwar na Mahathir waliweka kando tofauti zao na kuweka nguvu zao pamoja na kupambana na serikali hiyo iliyoingiliwa na ugonjwa wa rushwa katika uchaguzi wa mwaka 2018. Mahathir , ambaye aliwahi kuwa waziri mkuu kuanzia mwaka 1981 hadi 2003, alitoa ahadi ya kabla ya uchaguzi ya kukabidhi madaraka kwa Anwar lakini mara kwa mara alikuwa anakataa kuweka tarehe ya makabidhiano.
Muda mfupi kabla ya kujiuzulu , chama cha Mahathir cha Bersatu kilijitoa kutoka katika muungano unaounda serikali na wabunge kadhaa walijiuzulu kutoka katika chama cha Anwar, wakauacha muungano wa makubaliano ya matumaini katika hali mbaya na kuchochea fununu kuwa juhudi ziko mbioni kuunda ushirika mpya. Mahathir pia amejiuzulu kuwa mwenyekiti wa chama chake cha Bersatu.