Mswada wa mwisho wa mabadiliko ya tabia nchi kuwasilishwa
13 Desemba 2018Rais wa mkutano huo kutoka Poland anatarajiwa kuwasilisha mswada wa waraka wa mwisho ambao utajumuisha sheria maalum za utekelezaji wa makubaliano ya Paris, makubaliano juu ya kugharamia mabadiliko ya tabia nchi na mkataba mwingine wa kuongeza juhudi za kuzuwia utoaji wa gesi zinazochafua mazingira.
Mswada huo utawasilishwa kwa wajumbe na mawaziri watafanyakazi kuweza kupata waraka utakaoweza kukubalika ifikapo mwisho wa mkutano huo kesho Ijumaa. "Maelezo yanapaswa kuchujwa na tunapaswa kuangalia wapi tunakutana kwa vipande tofauti vya waraka huu, lakini hatujafika huko hadi sasa," amesema hivyo Jennifer Morgan, mkurugenzi mtendaji wa shirika la Greenpeace International.
"kila nchi hapa inahitaji kuchukua hatua moja nyuma na kukumbuka kwa nini tuko hapa. Uhai wetu uko hatarini.
Wajumbe kufikia makubaliano Katowice
Bado haijafahamika ni vipi wajumbe watakamilisha makubaliano ya utekelezaji wa makubaliano ya Paris, ambayo yanalenga kubakisha ongezeko la ujoto kuwa chini ya nyuzi joto mbili juu ya nyakati kabla ya enzi za viwanda, na iwapo waraka huo utatilia maanani ripoti ya hivi karibuni ya jopo la Umoja wa Mataifa linaloundwa na muungano wa serikali mbali mbali kuhusu mabadiliko ya tabia nchi IPCC.
Mataifa ambayo yanakabiliwa na athari kubwa za mabadiliko ya tabia nchi yametaka mkutano huo kutoa ujumbe mzito kwamba dhamira ya dhati ya kupunguza utoaji wa gesi zinazoharibu mazingira duniani ni lazima kuimarishwa ifikapo mwaka 2020.
Visiwa vya Maldives vitafanya kila linalowezekana katika uwezo wake kuzuwia maji kukimez kisiwa hicho, mkuu wa ujumbe wa nchi hiyo katika mkutano huo amesema leo katika hali ya kutoa wito kwa mataifa kuondoa tofauti zao kuhusiana na jinsi gani ya kupambana na ongezeko la ujoto duniani.
"Hatuko tayari kufa. Hatutakuwa wahanga wa kwanza wa mzozo wa mazingira. Badala yake , tutafanya kila kitu katika uwezo wetu kuweka vichwa vyetu juu ya maji," Mohamed Nasheed aliwaambia wajumbe katika mazungumzo hayo ya Katowice , nchini Poland.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Josephat Charo