Msumbiji yalaani ukatili wa mwanamke kuuawa, akiwa uchi
15 Septemba 2020Katika kanda ya video ambayo haijathibitishwa lakini ambayo ilisambaa mitandaoni jana Jumatatu, watu waliomuua mwanamke huyo, walimtuhumu kuwa mwanachama wa kundi liitwalo al-Shabaab, ambalo ni kundi la wanamgambo wenye itikadi kali za Kiislamu katika eneo hilo la kaskazini mwa jimbo la Cabo Delgado tangu mwaka 2017. Kundi hilo halina uhusiano na lile la Somalia, japo yana majina yanayofanana.
Kwenye video hiyo, mtu mmoja anaonekana akimcharaza bakora kichwani na kote mwilini huku wengine walioko upande mwingine wa barabara wakisema muue.
Msumbiji: Ugaidi waongezeka katika jimbo la Cabo Delgado
Kwenye taarifa iliyotolewa jana jioni, jeshi la Msumbiji (FDS) ambalo limekuwa likipambana na wanamgambo katika mkoa huo, limesema video hiyo ni ya kushangaza na kuhuzunisha na pia ni ya kulaaniwa.
Jeshi hilo limesisitiza kuwa halikubaliani na kitendo hicho cha ukatili ambacho kinakiuka haki za binadamu. Jeshi hilo limetaka uchunguzi kufanywa kuhusu uhalali wa video hiyo.
Vidio hiyo imejiri mnamo wakati kuna madai ya ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na wanajeshi mkoani Cabo Delgado, ambao pia ni makao ya miradi mikubwa ya uchimbaji gesi inayotekelezwa na kampuni kubwakubwa kama Total.
Baada ya ongezeko la machafuko ya wanamgambo na hata kuukamata mji mmoja muhimu wa bandari mnamo mwezi Agosti, huku kukiwa na makabiliano makali kutoka vikosi vya usalama vya serikali, ripoti na video nyingi kuhusu watu kupigwa au haki zao kukiukwa zimekuwa zikijitokeza kwa wingi.
Amnesty International yashutumu ukiukaji wa haki za binadamu Msumbiji
Wiki iliyopita, shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International, lilisema lilithibitisha kanda za video zilizoonyesha majaribio ya watu kuchinjwa, kuteswa na visa vingine vya kikatili dhidi ya wafungwa, ikiwemo kuwakata vipande washukiwa pamoja na uwezekano wa mauaji ya kiholela dhidi yao.
Serikali iliyapuuza na kuyakana madai hayo ikisema mara kwa mara wanamgambo, hujifanya kuwa wanajeshi kama hatua ya kuupumbaza umma pamoja na maoni ya kimataifa.
Soma pia: Wanajeshi wa Msumbiji kupambana na waasi
Zenaida Machado ambaye ni mtafiti wa shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, ametaka uchunguzi kufanywa akisema ikiwa visa hivyo vimefanywa na wanajeshi, basi inaongeza ukosefu wa imani miongoni mwa umma na pia inaimarisha nadharia au misimamo ya wanamgambo.
Zenaida amesema, kitendo hicho ni kiwango cha juu cha usaliti, akiongeza kuwa watu wenye hofu hawapaswi kukimbia kutoka kwa wanamgambo kisha mwishowe kujikuta kwenye hatari mikononi mwa wale wanaopaswa kuwapa usalama.
(RTRE,AFPE)