Msiba mmoja baada ya mwingine Syria, maafa yazidi
21 Julai 2012Waasi wameyashambulia makambi ya wanajaeshi wa serikali mjini Damascus na kuzidisha kizaazaa, kilichodumu kwa siku ya sita mfululizo. Huku hayo yakiarifiwa televisheni ya kitaifa nchini humo leo imethibitisha kufariki kwa mkuu wa ujasusi wa Syria, Hisham Ikhtyar.
Muda mfupi uliopita, serikali ya Syria, kupitia televisheni yake ya taifa, imethibitisha kifo cha mkuu wa ujasusi, Hisham Ikhtyar, aliyejeruhiwa katika shambulio la jumatano katika makao makuu ya jeshi na usalama wa taifa.
Kizaazaa chapamba moto mjini Damascus
Katika tukio lingine, moshi mkubwa umeonekana ukifuka kutoka katika mabaki ya nyumba na majengo yaliyoshambuliwa mjini Damascus leo, huku maiti tatu zikiwa zimejaa damu katika viunga vya Midan, wilaya iliyowekwa tena chini ya ulinzi na vikosi vya serikali ya Syria, baada ya makabiliano makali baina yake na waasi.
Kwa mujibu wa maelezo ya televisheni ya taifa mapema leo asubuhi, vikosi vya serikali vimeusafisha mji wa Medan, kauli inayomaanisha kwamba askari wanaomtii Rais Assad wamewavamia na kuwashughulikia wapinzani, ambao utawala huo unawaita magaidi.
Kama vile haitoshi, chombo hicho cha serikali kimeonesha pia picha za wafungwa wakiwa na pingu mikononi na uharibifu uliotokea, kufuatia makabiliano hayo.
Kwa mara ya kwanza tangu vuguvugu la kumpinga Assad lianze miezi 16 iliyopita, televisheni hiyo ya faita imeonesha picha za miili ya waasi waliouwawa mjini Damascus, bila kutaja lakini ni wapi mauaji hayo yametokea.
Vilevile, Jeshi la Syria limearifu kuwa kiwango kikubwa cha silaha, yakiwemo maroketi na vifaa vya mawasiliano, vimekamatwa mjini Midan, baada ya kuvamia eneo hilo linaloficha wapinzani.
Je ni kweli wapinzani wamesalimu amri Syria?
Mwanaharakati mmoja anayejiita Ahmed Midani, amesema na hapa na mnukuu" Jeshi huru la Syria limeondoka Midan usiku wa kuamkia leo kwa sababu ya mapambano makali."
Ahmed ameongeza kusema kuwa waasi hao wamewachukua pia wanawake 200 pamoja na watoto ili kuwaepusha kubakwa ama kuuwawa na askari wa Assad. Bado upekuzi unaendelea katika nyumba za mjini hapo na watu wanatiwa nguvuni.
Kufuatia kadhia hiyo, baada tu ya sala za Ijumaa, watu walitoka misikitini na kuingia barabarani wakiandamana kupinga uhalifu huo.
Akiwa mjini Roma, Italia, Mwenyekiti wa Baraza la Kitaifa la Syria, AQbdulbaset Sieda amesema ..."Tumezungumzia juu ya hali ya kisiasa na ile kura ya turufu iliopigwa na Urusi katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Kutokana na muktadha huo, nasema mambo hayawezi kuendelea kama yalivyo sasa. Urusi inauunga mkono utawala wa Syria kwa silaha, vifaru, mizinga na maroketi pamoja na ndege za kivita, na silaha hizo zinatumiwa kuwaangamiza watu wetu. Na zaidi ya hayo, Urusi inaulinda utawala wa Syria katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa."
Taarifa kutoka mjini Aleppo, mji wa pili kwa ukubwa nchini Syria, zinasema kuwa vikosi vya serikali vimewashambulia waandamanaji hii leo, na jumla ya watu watano wamepoteza maisha. Kati ya hao ni raia wawili na waasi watatu.
Mwandishi: Ndovie, Pendo Paul\AFP
Mhariri: Miraji Othman